Main Title

source : Parstoday
Jumatano

31 Januari 2024

20:03:10
1434107

Wakulima wenye hasira waandamana barani Ulaya kupinga sheria za EU

Wakulima wenye hasira wanaendelea na maandamano kote katika Umoja wa Ulaya kupinga kushuka kwa mapato na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Hali ya kutoridhika imeenea miongoni mwa wakulima kote barani Ulaya ambapo wamefunga bandari na barabara katika wiki za hivi karibuni kulalamikia bei ya chini ya bidhaa, kanuni za kilimo za Umoja wa Ulaya (EU), na ushindani usio wa haki kutoka kwa bidhaa za bei nafuu.

Siku ya Jumanne, wakulima wa Ufaransa, wakiendeleza maandamano kwa zaidi ya wiki mbili, walifunga barabara kuu kwa kutumia matrekta yao karibu na Paris na kuzuia wasafiri kufika uanja wa ndege wa Toulouse. Wanalalamikia malipo duni ya bidhaa zao na sheria kali kupindukia ya EU juu ya ulinzi wa mazingira.

Huko Italia, wakulima walikusanyika kwa siku ya tatu mfululizo wakiwa na matrekta yao kwenye njia ya karibu na Roma siku ya Jumanne, ili kutetea sekta ya kilimo ya Italia.

Walipinga sera za kilimo za EU, kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, ushuru wa juu na mapato ya chini, na kupunguzwa ruzuku ya dizeli.

Nchini Ubelgiji wakulima wanaoandamana waliendelea kufunga barabara jana Jumanne wakiahidi kuendeleza maandamano hayo iwapo matakwa yao hayatatekelezwa na serikali yao.Wengi wanasema waandamanaji wanalenga kuelekea makao makuu ya Umoja wa Ulaya, Brussels, kesho Alhamisi, siku ambayo viongozi wa Umoja wa Ulaya watakusanyika katika mji huo kwa ajili ya mkutano uliopangwa awali. Nyaya na vizuizi vimewekwa karibu na Bunge la Ulaya huko Brussels wakati wakulima wanaoandamana walipokusanyika karibu na eneo hilo. Wakulima wa Uhispania wamesema watajiunga na harakati na kuandaa maandamano mwezi ujao wa Februari. EU ilifuta ushuru wa baadhi ya bidhaa za kilimo zinazoingia barani humo baada ya Russia kuanza operesheni yake maalumu ya kijeshi nchini Ukraine. Wakulima wa Ulaya pia wanakerwa na kuanza upya mazungumzo ya kuhitimisha makubaliano ya kibiashara kati ya EU na kambi ya Amerika Kusini ya Mercosur. Wakulima aidha wanasema mapato yao duni yanatokana na sera kali za kimazingira hasa marufuku ya kemikali zinazotumika katika kilimo.  

342/