Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

3 Februari 2024

19:37:22
1434896

Wamarekani waandamana kupinga himaya ya Washington kwa jinai za Israel huko Gaza

Wananchi wa Marekani wamefanya maandamano makubwa wakipinga uungaji mkono na himaya ya serikali ya Washington kwa jinai na mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kutaka kusitishwa mara moja vita huko Palestina.

Waandamanaji hao wa Marekani, wakiwa wamebeba mabango yanayotaka kukomeshwa uungaji mkono wa Ikulu ya White House kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, wametaka kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza.

Mamia ya Waislamu na Wamareka wenye asili ya Kiarabu wanaoishi katika jimbo la Michigan pia wamejitokeza mabarabarani wakati wa ziara ya Rais Joe Biden wa Marekani katika jimbo hilo kueleza malalamiko yao dhidi ya sera zake za kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza.

Maandamano hayo ya wananchi ya kupinga uungaji mkono na misaada ya Washington kwa jinai za Israel, yameshamiri huku hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza ikizidi kuwa mbaya kila siku kutokana na kimya cha madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.

Katika muktadha huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limeonya kuwa huenda likalazimika kusimamisha shughuli zake katika eneo lote la Asia Magharibi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Februari kufuatia shutuma za Israel dhidi ya wafanyakazi 12 wa shirika hilo na kusimamisha misaada ya nchi za Magharibi kwa UNRWA.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameziomba nchi za dunia kuendelea kuchangia misaada ya kifedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kutokana na hali mbaya inayoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza kwa sababu ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni.

342/