Main Title

source : Parstoday
Jumanne

6 Februari 2024

15:24:40
1435780

"Akthari ya madini yanayohitajika na sekta ya nishati duniani yapo Afrika"

Rais wa Afrika Kusini amesema aghalabu ya madini ya thamani yanayohitajika katika mageuzi makubwa kwenye sekta ya nishati duniani yanapatikana katika ardhi ya Afrika.

Cyril Ramaphosa amesema hayo katika hotuba yake kwenye kongamano kubwa zaidi la madini maarufu kwa jina la  "Mining Indaba" linalofanyika jijini Cape Town na kuongeza kuwa: Madini muhimu ya manganese, chuma, shaba nyekundu, kobalti (cobalt), nikeli (nickel), na platinum yote yanapatikana katika ardhi yenye utajiri ya Afrika.

Amewataka viongozi wa Afrika kuchukua hatua za makusudi za kuhakikisha kunapatikana maendeleo na ustawi mkubwa katika sekta za madini za bara hilo.

Ramaphosa ameeleza bayana kuwa, uekezaji mkubwa katika utafutaji madini utainua uchumi wa nchi za Afrika na kuwavua watu wa bara hilo kutoka kwenye umaskini na kuwajengea mazingira mazuri ya utajiri na ustawi wa kijamii.

Kongamano hilo la kila mwaka la 'Mining Indaba' ambalo linawaleta pamoja wawekezaji na wataalamu wa madini kutoka kona mbali mbali za dunia mjini Cape Town, linaadhimisha miaka 30 tangu kuasisiwa kwake.Si vibaya kuashiria hapa kuwa, shughuli za uchimbaji madini katika aghalabu ya migodi ya nchi za Afrika zinafanyika kinyume cha sheria na bila ya uangalizi wa vyombo vya dola. Takwimu zinaonyesha kuwa, aghalabu ya madini yenye thamani hususan ya dhahabu na almasi yanayochimbwa kinyume cha sheria katika nchi za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.

342/