Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

8 Februari 2024

06:33:19
1436116

Malengo ya kubaathiwa Mtume Muhammad SAW

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Leo hatutokuwa na kipindi cha BLW na badala yake tumekuandalieni makala maalumu ya kuzungumzia kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW. Hii ni siku muhimu sana katika ulimwengu mzima.

Leo makala yetu itajikita katika maudhui ya malengo ya kutumwa Bwana Mtume Muhammad SAW awe rehema kwa walimwengu wote. Ni wazi kuwa hatuwezi kuzungumzia malengo yote katika kipindi hiki cha dakika chache, lakini tutajitahidi kugusia yaliyo muhimu zaidi katika suala hili zima la kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW. Dunia imejaa matatizo leo hii kutokana na wanadamu kutojali na kutofuata mafundisho sahihi aliyokuja nayo Bwana Mtume Muhammad SAW. Karibuni.

Wasikilizaji wapenzi, katika siku za kukaribia tarehe 27 Rajab, Mtume Muhammad SAW alikuwa akienda katika pango la Hiraa na katika baadhi ya nyakati alikuwa akikaa siku kadhaa katika eneo hilo. Alikuwa akimfahamisha mke wake mtiifu Khadija kuwa: ‘Wewe pia wafahamu mahaba na mafungamano yangu. Katika siku hizi nina hisia ya ajabu ya kupenda kumkumbuka Mola Muumba, moyo wangu hautaki chochote isipokuwa hilo.’

Hatimaye usiku uliojaa siri uliwadia. Mwezi uliangazia nuru yake katika eneo la kusini la mlima.  Kulikuwa na kimya mutlaki na cha ajabu katika kila sehemu. Ilikuwa ni kana kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zinasubiri tukio adhimu.

Mtume Muhammad SAW alikuwa akikesha katika aghlabu ya nyusiku. Hakuna sauti iliyokuwa ikisikika katika milima usiku huo. Kimya na utulivu wa usiku huo ulikuwa na maana maalumu. Katika lahadha hiyo iliyojaa siri kubwa, nuru kutoka mbinguni iliangazia upeo wa Mtume Muhammad SAW. Alihisi mtikisiko katika mwili na roho yake. Katika lahadha hiyo, ghafla kiumbe adhimu alijitokeza mbele ya macho ya Muhammad. Alikuwa kiumbe mwenye adhama na utukufu. Kila upeo alioangalia katika mbingu, Muhammad alimuona kiumbe huyo aliyejaa nuru. Alikuwa ni Malaika wa Wahyi, Jibril AS. Hapo Jibril alimkaribia Muhammad na kunena ifuatavyo.

Ewe Muhammad Soma. Muhammad alitazama kwa makini.  Aliona maandishi mbele ya uso wake. Kwa mara nyingine sauti ikaja na kusema, ‘Soma kwa jina la Mola wako Mlezi. Kwa sauti ya iliyotikisika, Muhammad aliuliza, Je nisome nini? Sina ujuzi wa kusoma. Hapo malaika alisema:

Soma kwa jina la Mola Wako aliyeumba. Amemuumba mtu kwa pande la damu. Soma! Na Mola Wako ni Karimu Zaidi!  Ambaye amefundisha kwa kalamu. Amemfundisha mtu aliyokuwa hayajui. Surat Al-`Alaq (1-5).Mtume Muhammad SAW, ambaye uwepo wake wote ulikuwa unabubujika mahaba ya mbinguni, alianza kusoma na Malaika Jibril AS.

Kwa mara nyingine Muhammad alisikia sauti ikimwambia: ‘Ewe Muhammad wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu’ Hii haikuwa ndoto, bali lilikuwa ni tukio la kweli.  Naam, alikuwa katika irada ya Mwenyezi Mungu na kupata taufiki ya kuwa mja ambaye Mwenyezi Mungu alizungumza naye. Mwenyezi Mungu SWT alimteua Muhammad SAW miongoni mwa viumbe wengine na alimtambua kama mwenye ustahiki wa kupokea Wahyi. Mtume Muhammad SAW ambaye daima alikuwa akiwaza na kutafakari kuhusu namna ya kuwaokoa watu kutoka katika upotofu, hivi sasa alikuwa na jukumu adhimu.

Alipata hisia za ajabu katika mwili na roho yake. Alihisi joto kali sana. Mabega yake yalitikisika kwa msisimko aliokuwa nao. Alitaka kusimama kutoka sehemu aliyokuwepo. Hata hivyo alihisi kutokuwa na uwezo. Hapo alianguka chini kifudifudi bila hiyari na alianza kutokwa na machozi. Katika usiku huo uliojaa msisimko yaani mkesha au usiku wa kuamkia mwezi 27 Rajab, Muhammad SAW aliteuliwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mitume wote wa Mwenyezi Mungu wametumwa kama yeye ili waweze kumuongoza mwanaadamu kutoka katika kiza cha ujahili na shaka na kuwapelekea katika nuru ya elimu na maarifa. Tab’an kila Mtume alitumia mbinu maalumu za kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa kutegemea hali na zama alizoishi.

Amma suala muhimu na lenye taathira katika kuenea mafundisho aliyokuja nayo Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW ni shakhsia yake muhimu pamoja na sifa za kipekee za ujumbe wake.

Yaliyomo katika Aya za Qur’ani Tukufu ni mjumuiko wa maarifa yenye mafunzo muhimu na yenye thamani kubwa. Maarifa ya Qur’ani Tukufu yanaenda sambamba na akili na pia kuondoa utata uliomo katika akili za watu. Sifa hizo za kipekee za Qur’ani Tukufu ndicho chanzo cha wenye kutafuta haki kuvutiwa na kuamua kufuata Uislamu.

Mtume Muhammad SAW, alibainisha na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu ujumbe wake kwa kutumia mantiki, dalili za wazi na kwa ufasaha wa hali ya juu. Alifafanua kikamilifu na kwa uwazi kuhusu kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja. Naam, Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi na vyote vilivyomo humo.

Mtume SAW daima alikumbusha kuhusu ishara za kuwepo Mwenyezi Mungu katika maumbile ya dunia na hivyo kupelekea watu wamzingatie Mola Muumba. Alibainisha kuwa, dunia imeumbwa kwa msingi wa nidhamu maalumu na erevu.

Katika ujumbe wake, Mtukufu Mtume Muhammad SAW alibainisha ufahamu kuhusu nukta kama vile kutafuta ukweli, kusimamia uadilifu na kuwepo uhusiano mzuri na salama baina ya wanaadamu. Mafundisho aliyobainisha Mtume SAW ni mafunzo yaliyoenda sawia na maumbile asilia na fitra ya mwanadamu. Watu waliokuwa na masaibu katika zama hizo za kudhihiri Uislamu waliweza kupata uhai mpya kutokana na mafundisho ya Mtume Muhammad SAW ambaye aliwapa bishara njema za maisha mazuri na yenye furaha na ufanisi. Ni wazi kuwa iwapo maarifa ya Uislamu hayakuwa na sifa za kipekee basi dini hii haingeweza kuenea miongoni mwa walimwengu. Ujumbe wa Mtume SAW uliweza kupenya na kukita mizizi katika nyoyo za watu walioukubali Uislamu na kuufuata.

Kati ya nukta muhimu katika itikadi ya Kiislamu na ambayo pia ilikuwa moja ya malengo ya juu ya kubaadhiwa na kutumwa Mtume Muhammad SAW ni elimu na malezi.  Mtume Muhammad SAW alifuatilia na kusisitizia sana wajibu kueneza elimu na maarifa sambamba na malezi bora ya kiroho. Qur’ani Tukufu katika aya pili ya Surat al Jumua inaashiria malengo ya Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW kama ifuatavyo:

"Yeye Ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, aliyetokana na wao, awasomee Aya Zake, na awatakase, Na awafunze Kitabu na hikima, Japokuwa hapo kabla walikuwa katika upotofu ulio dhahiri."

Kwa msingi huo, Mtume Muhammad SAW alikuwa na jukumu la kusoma aya hizo za Mwenyezi Mungu ambazo huinua hadhi ya mwanaadamu ili kutakasa nafsi za watu na kuwaondoa katika dimbwi la upotofu wa shirki na itikadi batili ili waweze kuwa ni wenye akhlaqi na maadili bora. Katika kubainisha lengo hilo Mtume Mtukufu Muhammad SAW amenukuliwa akisema: “Hakika mimi sikutumwa ila kukamilisha maadili mema”

Kwa hivyo kati ya malengo muhimu ya kubaathiwa Mtume wa Mwisho, Muhammad al Mustafa SAW yametajwa katika Qur'ani Tukufu kuwa ni pamoja na kutakasa nafsi na kuwalea wanaadamu ili waweze kustawi na kufikia daraja la juu la ukamilifu wa mwanadamu. Ni katika kivuli hiki ndio maana uhusiano wa mwanadamu na Muumba hurekebishwa katika jamii ya Kiislamu.

Mtume Muhammad SAW si tu katika maneno, bali pia katika vitendo, alikuwa kigezo bora zaidi kwa wanadamu katika nyuga zote ukiwemo upeo wa maadili mema. Mtukufu huyo aliwaongoza watu na kuwa mfano wa kuigwa na wengine katika utekelezaji mafundisho na ibada za Kiislamu. Hulka njema na tabia iliyojaa ukarimu ya Mtukufu huyo miongoni mwa watu ni nukta ambazo zilikuwa na mvuto wa kipekee.

Taathira hii ya kipekee ya akhlaqi na maadili bora za Mtume Muhammad SAW ndio nukta ambayo ilipelekkea Waarabu wa zama za ujahiliya au ujinga wakubali kuwa karibu mno na mtukufu huyo ili waweze kupata mafundisho ya muongozo wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa mwanadamu huyo ambaye ni mbora wa viumbe wote wa Mwenyezi Mungu kwa umbo na kwa tabia.

Katika zama za Risala ya Mtume wa Uislamu SAW, kipindi kigumu zaidi kilikuwa ni wakati wa jitihada za kubadilisha na kuondoa itikadi potofu za Waarabu na ushirikina. Aghlabu ya Waarabu walikuwa ni watu wenye taasubu sana. Sasa ili kupata mafanikio katika kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu SWT katika mazingira hayo magumu, Mtume Mtukufu SAW alitegemea nukta muhimu sana, nayo ni maadili bora.

Mtukufu huyo aliheshimu shakhsia ya mwanadamu hata ya watu waliokuwa na taasubu. Alijitahidi kuhakikisha kuwa kunapatikana mazingira tulivu na yasiyo na utata ili aweze kueneza ujumbe aliotumwa na Mwenyezi Mungu kuufikisha.  Mtume SAW hata alijiepusha kuwadhalilisha watu majahili au wajinga na kila alipolazimika kuingia katika mdahalo hakuwa akiwakejeli na alikuwa akitafuta fursa muafaka ya kuendeleza mazungumzo nao. Katika kufikisha ujumbe wa haki, Mtume SAW aghlabu ya wakati alikuwa akianzia katika nukta ambayo inakubaliwa na upande wa pili. Alitumia sana mbinu hii katika midahalo yake ni Ahlul Kitab.

Mtume Muhammad SAW alikuwa akizingatia kwa kina uwezo wa ufahamu wa kila mtu na ni baada ya hapo ndipo alikuwa akibainisha msimamo wake.

Mtume Mtukufu SAW alikuwa na uhusiano na watu wa matabaka ya rika na daraja za kila namna. Ujumbe wa mtukufu huyo uliwalenga wazee, vijana, wanaume, wanawake, masikini, matajiri, wenye elimu na wasio na elimu na watu wote tu.

Wakati Mtume SAW alipokuwa akiwahutubu Ahlul Kitab, alikuwa akianza na nukta za pamoja baina ya dini zao na Uislamu. Baadhi ya wakati tabasamu tamu na mtazamo wa kina kwa jicho la Mtukufu huyo ni jambo ambalo lilivutia nyoyo na kuwa na ushawishi kamili kwa hadhirina ambao walipata muongozo kupitia mafundisho yake ya haki na yenye kutoa muongozo.

Mtume Mtukufu SAW daima alijitahidi kuwafikishia wanaadamu ujumbe wa haki katika kivuli cha kumcha Mungu Moja, Muumba wa Mbingu na Ardhi. Ni kwa msingi huo ndio maana moja ya nara na kauli mbiu aliyotumia ni: ‘Sema Hakuna mungu Apasaye Kuabudiwa ila Mungu Moja ili ufanikiwe’.

Hivi sasa na katika siku hizi zilizojaa masaibu, tunashuhudia Waislamu na wasio kuwa Waislamu wasio na hatia wakiuawa kiholela mikononi mwa watu makatili na wasio na hisia za utu, sawa kabisa na ilivyokuwa katika zama za ujahiliaya.

Kumbukumbu ya kubaathiwa Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad Al Mustafa SAW ni fursa nzuri ya kuzingatia kwa kina na kufuata mafundisho yenye kuleta saada ya Uislamu na sira tukufu ya mtukufu huyo.

Kwa hakika Maarifa ya Qur’ani Tukufu, Sira ya Mtume SAW na Ahul Bayt wake ni taa na nuru za kuwaondoa watu waliomo kwenye kiza za ujahili au ujinga za zama hizi na kuwaingiza katika nuru ya uongofu.

Naam, wasikilizaji wapenzi, lau kama walimwengu watazingatia na kufuata kivitendo mafundisho matukufu ya Manabii na Mitume wa Mwenyezi Mungu wakiongozwa na Mtume Muhammad SAW, basi si tu watapata mafanikio ya hapa duniani, lakini wataokoka pia na mabalaa ya Siku ya Kiyama. Tunamuomba Allah atufanikishe kufuata kivitendo mafundisho ya uongofu wetu wa duniani na Akhera. Aamin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.342/