Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

10 Februari 2024

14:28:55
1436651

Meta yafunga kurasa za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kwenye Instagram, Facebook

Kampuni ya Kimarekani ya Meta Platforms, Inc. inayoendesha na kumiliki Instagram, imefunga akaunti za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook.

Meta Platforms, ambayo ilifanya kazi kwa jina la "Facebook" hadi 2021, ilidai Alhamisi iliyopita kwamba akaunti za Ayatullah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Iran, kwenye Instagram na Facebook zimefutwa kwa sababu ya ukiukaji wa sera za kampuni hiyo katika uwanja wa mashirika na watu hatari. Akaunti za kurasa za mtandaoni za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hapo awali pia zilikabiliwa na vikwazo na kufutwa kwenye majukwaa kama vile Instagram na Twitter (sasa X). 

Hatua ya sasa ya Meta imekuja kufuatia miezi kadhaa ya mashinikizo ya makundi yanayounga mkono utawala mtendajinai wa Israel, ambayo yanajulikana kwa kuwa na ushawishi mkubwa katika maamuzi ya makampuni mbalimbali ya Marekani.

Akaunti hizo za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu zimefutwa baada Ayatullah Khamenei kusema, maafa yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza ni janga kwa ulimwengu wa Kiislamu na ubinadamu kwa ujumla. Vilevile alitoa wito kwa mataifa ya Kiislamu kukata uhusiano wao na Israel hususan uhusiano wa kiuchumi, suala ambalo limepongezwa na kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa katika mitandao ya kijamii.Meta imekuwa ikikiuka uhuru wa kujieleza kwa kuondoa maudhui zinawazotetea Wapalestina kwenye Instagram na Facebook, tangu Oktoba 7, 2023, wakati utawala wa Israel ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Hatua ya makampuni ya Magharibi ya kufunga akaunti za Kiongozi Muadhamu kwenye mitandao ya kijamii ya Meta zenye mamilioni ya wafuasi katika maeneo mengi ya dunia inaonyesha uadui wa wazi wa nchi za Magharibi dhidi ya uhuru wa kujieleza. Akaunti za Kiongozi Muadhamu zimezuiwa katika hali ambayo, katika miaka ya hivi karibuni shakhsia, maafisa na hata raia wa kawaida wa nchi za Magharibi wametumia mitandao hiyo ya kijamii kuhamasisha na kuunga mkono chuki dhidi ya Uislamu, kukitukana kitabu kitukufu cha Waislamu na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) kwenye mitandao ya kijamii bila ya kuchukuliwa hatua yoyote. Kuwaunga mkono watu na makundi yanayohujumu dini ya Uislamu yenye wafuasi wapatao bilioni mbili katika mitandao ya kijamii kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza katika nchi za Magharibi ni kielelezo kingine cha mgongano na sera za kinafiki za nchi za Magharibi kuhusiana na madai ya kutetea uhuru wa kujieleza na haki za binadamu. 

Ijapokuwa uhuru wa kusema ni miongoni mwa mambo yanayopigiwa upatu na madola ya Magharibi lakini tajriba imethibitisha kwamba Wamagharibi wanaukubali uhuru wa kujieleza katika uga wa kisiasa pale unapolinda na kudhamini maslahi na sera zao. Mkabala wake, Uislamu, pamoja na kutilia mkazo uhuru wa binadamu, hautofautishi baina ya wanadamu kwa msingi wa rangi, dini na mbari zao. 

Baada ya kushindwa mtawalia utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani katika makabiliano ya hivi karibuni na wapiganaji wa Palestina na waungaji mkono wa mapambano ya ukombozi wa Wapalestina, ilitabiriwa kuwa ubeberu na Uzayuni vitatumia kila mbinu kushambulia azma ya wananchi wa Palestina na watetezi wao. Kukatwa misaada ya nchi za Magharibi kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) na kuzuiwa kwa tovuti ya Kiongozi Mkuu wa Iran kama muungaji mkono muhimu zaidi wa haki za watu wa Palestina, vinatathminiwa katika mkondo huo. 

Hatua ya kampuni ya Meta ya kufunga kurasa za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram ni mfano wa wazi wa unafiki na sera za kindumakuwili za Magharibi kuhusu uhuru wa kujieleza, na inapaswa kutambuliwa kama hatua ya kuushajiisha utawala wa Kizayuni wa Israel kutenda jinai zaidi huko Gaza. Utawala huo umefanya uhalifu usio na kifani na hadi sasa umeua Wapalestina 28,000 na uharibifu wa 80% ya nyumba na miundombinu ya Gaza.

Hata hivyo uzoefu wa miaka 45 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran umeonyesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu na viongozi wake hususan Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kamwe hawatatishwa na vikwazo, vitisho na mashinikizo ya aina yoyote katika njia ya kupigania haki na uhuru wa nchi, watu wa Iran na mataifa mengine yanayodhulumiwa kama Palestina.



342/