Main Title

source : Parstoday
Jumapili

11 Februari 2024

19:17:15
1436865

Iran inaadhimisha miaka 45 ya ushindi ya Mapinduzi ya Kiislamu

Wananchi wa Iran leo wanaadhimisha miaka 45 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyotokea 1979.

Leo Jumapili tarehe 22 Bahman, sawa na tarehe 11 Februari, wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanaadhimisha sherehe za miaka 45 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.

Katika sherehe hizo mamilioni ya wananchi wa taifa hili wanatarajiwa kumiminika mabarabarani katika maandamano ya amani ya kumbukumbu ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, ambapo kwa mara nyingine watajadidisha kiapo cha utiifu kwa Imamu Khomein, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kadhalika Wairan watatangaza utiifu wao kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamedumu kwa miongo minne na nusu licha ya njama za Marekani na washirika wake za kutaka kuyasambaratisha mapinduzii haya. 

Ikumbukwe kuwa, miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote. Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung’oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi. Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu.

\342/