Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

12 Februari 2024

19:25:50
1437181

Iran: Israel haina uwezo wa kuendeleza vita Gaza hata kwa siku 1 bila ya uungaji mkono wa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, iwapo Marekani itaacha kuuunga mkono utawala wa Kizayuni, utawala huo hautoweza kuendeleza vita dhidi ya Gaza hata kwa siku moja.

Amir-Abdollahian, ambaye yuko ziarani nchini Syria, jana Jumapili alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Bashar Assad wa nchi hiyo. Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema mgogoro wa Gaza ndio suala kuu katika ngazi ya kimataifa na akaashiria msimamo wa pamoja wa Iran na Syria katika kuunga mkono suala la Palestina na kusema: vita si suluhisho la kadhia ya Gaza na mauaji ya kimbari ya Wapalestina inapasa yakomeshwe mara moja. Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, ikiwa Marekani ni mkweli katika madai yake kwamba haina nia ya kupanua wigo wa vita katika eneo, inapaswa isimamishe uungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni. Mwanadiplomasia mkuu wa Iran ameeleza bayana kwamba: "tunaamini kuwa viongozi wa makundi ya Palestina na wananchi wa Palestina wanao uwezo wa kupitisha maamuzi kwa ajili ya uendeshaji wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan baada ya vita, kwa sababu Muqawama wa Palestina ungali imara na wenye nguvu.

Katika mazungumzo hayo, Rais Bashar Assad wa Syria  ameupongeza uongozi, serikali na wananchi wa Iran kwa mnasaba wa kaudhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na akaeleza kwamba: kile ambacho Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekifanya katika kipindi cha miezi minne iliyopita katika kuiunga mkono Palestina, kimeuthibitishia ulimwengu kwa mara nyingine kuwa Iran haisemi maneno matupu bali inatenda.

Aidha, Bashar Assad alisisitiza kuwa uungaji mkono wa Syria kwa muqawama na Palestina ni msimamo wa kihistoria na muqawama umekita mizizi nchini Syria na sera hiyo haitabadilika.Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuhudhuria mkutano wa pamoja na waandishi wa habari pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Miqdad, kuhutubia sherehe za madhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kuzuru haram tukufu ya Bibi Ruqyah (AS) ni ratiba zingine alizokuwa nazo Amir-Abdollahian katika safari yake hiyo nchini Syria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana pia na baadhi ya viongozi wa makundi ya muqawama ya Palestina na kuzungumzia matukio yanayojiri Gaza na ulazima wa kusimamishwa jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza.../

342/