Main Title

source : Parstoday
Jumatano

14 Februari 2024

14:20:03
1437736

Waziri wa Ulinzi wa Iran: Tuko tayari kufanya mazungumzo ya pamoja ya ulinzi na usalama na Saudi Arabia

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Iran iko tayari kufanya mazungumzo ya pamoja ya ulinzi na usalama na Saudi Arabia.

Brigedia Mohammad Reza Ashtiani, Waziri wa Ulinzi wa Iran ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Abdullah bin Saud Al-Anzi, balozi wa Saudi Arabia mjini Tehran na kueleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu na Saudia ni nchi mbili za Kiislamu na wadau wawili muhimu katika kulinda usalama na utulivu wa kanda ya Magharibi mwa Asia. Ameongeza kuwa: Suala la kustawishwa uhusiano na maingiliano yenye kujenga na nchi za eneo hili limesisitizwa katika siasa za nje za serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Brigedia Ashtiani amelitaja suala la Palestina kuwa ni kadhia nambari moja ya Ulimwengu wa Kiislamu na dunia nzima na kuongeza kuwa: "Kuna ulazima kwa nchi za Kiislamu, hususan nchi muhimu za eneo hili, kuchukua misimamo ya pamoja na madhubuti katika suala hilo, kama wajibu wao wa kidini na kibinadamu.

Waziri wa Ulinzi wa Iran ameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel kamwe hautafikia malengo yake huko Gaza na kusema, uingiliaji kati na himaya ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Isarel unaweza kutatiza hali ya usalama katika kanda ya Magharibi mwa Asia na kusababisha mgogoro mkubwa zaidi.

Ashtiani amesema nchi za Ghuba ya Uajemi zina maslahi na vitisho vinavyofanana na kuongeza kuwa, kuishi pamoja kwa amani na maelewano ni muhimu sana kwa suala zina la usalama wa kikanda.

Ametangaza utayarifu wa Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kustawisha ushirikiano wa kiulinzi, kijeshi na kiufundi na Saudi Arabia na kueleza kuwa, ushirikiano huo  utaboresha usalama na utulivu katika kanda hii.

Kwa upande wake, Abdullah bin Saud Al-Anzi, balozi wa Saudia nchini Iran sambamba na kusisitiza haja ya kustawishwa ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali zikiwemo nyanja za kiulinzi na kiufundi, amesema kuwa Iran na Saudi Arabia ni marafiki na ndugu, na kwamba mazungumzo ya wajumbe wa pande mbili na mikutano ya maafisa wa ulinzi vitaimarisha zaidi uhusiano wa nchi mbili.

342/