Main Title

source : Parstoday
Jumatano

14 Februari 2024

14:21:52
1437739

Kuongezeka ukosoaji wa Magharibi dhidi ya himaya ya Marekani kwa Israel katika vita vya Gaza

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, Jumatatu iliyopita aliitaka Marekani kuacha kutoa silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kiwango kikubwa cha mauaji ya raia katika vita vya Gaza.

Baada ya kikao chake na  mawaziri wa nchi za Umoja wa Ulaya huko Brussels, Borrell aliwaambia waandishi wa habari kuwa: "Ikiwa unaamini kwamba watu wengi watauawa huko Gaza, labda unapaswa kutoa silaha chache ili kuzuia watu wengi wasiuawe." Mkuu huyo wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya sambamba na kuitaka Marekani itazame upya sera zake za kutoa misaada ya silaha kwa Israel amesisitiza kuwa "Ikiwa jamii ya kimataifa inaamini kuwa haya ni mauaji na watu wengi wanauawa, labda inatupasa kutafakatri vyema kuhusu suala la kuipatia silaha Israel." Afisa huyo wa Umoja wa Ulaya ameongeza kuwa, ni hatua inayokinzana kwa nchi kutangaza mara kwa mara kwamba Israel inaua idadi kubwa ya raia huko Gaza lakini haichukui hatua yoyote muhimu kwa ajili ya kuzuia mauaji hayo.

Marekani ni mdhamini muhimu wa silaha za Isreal na kila mwaka hutoa misaada ya kijeshi yenye thamani ya dola bilioni 3.8 kwa Tel Aviv ikiwa ni pamoja na ndege za kivita na mabomu yenye nguvu kubwa; na hadi sasa Washington imekataa ombi lolote la kusimamisha au hata kukata misaada hiyo ya kijeshi kwa Isreal. Hii ni pamoja na kuwa, katika kipindi cha vita vya Gaza Marekani imeupatia utawala katili wa Israel kiwango kikubwa cha mabomu yanayopasua mgome za chini ya ardhi, na mabomu hayo yametumiwa kuwashambulia wakazi wa Gaza na  kuharibu miundombinu ya ukanda huo.

Matamshi hayo ya Borrell yametolewa baadea ya Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye ni muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vya Gaza, kukiri kwamba mashambulizi ya kijeshi ya utawala huo haramu huko Gaza yalivuka  mipaka. Rais Biden pia amesema katika mazungumzo yake na Mfalme wa Jordan kuwa idadi kubwa ya raia wa Palestina, wakiwemo wanawake na watoto, wameuwawa shahidi huko Gaza. Kauli hiyo ya rais Marekani imekuja wakati anakabiliwa na mashinikizo mengi yanayomtaka asitishe vita huko Gaza, na yeye mwenyewe anaelewa vyema athari za mashinikizo hayo juu ya wapiga kura kati ya wafuasi wa Chama chake cha Demokrasia. Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni nchini Marekani ambao ulifanywa hivi majuzi yanaonyesha kuwa vita vya Gaza vina taathiri kubwa katika kura za Joe Biden  kuliko propaganda zinazofanywa na mpinzani wake mkuu, Donald Trump. Nukta muhimu ni kwamba, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo mpya wa maoni, nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Inaonekana kuwa kuendelea vita vya Gaza na kuongezeka idadi ya mashahidi na majeruhi Wapalestina wanaoishi Gaza ambao kwa sasa wamepindukia watu laki moja, kumewafanya hata washirika wa Kimagharibi wa Tel Aviv, ukiwemo Umoja wa Ulaya, kukosoa mauaji hayo kwa kuzingatia kwamba utawala huo haramu unaendeleza mauaji ya kimbari kwa mwezi wa tano sasa dhidi ya watu madhulumu na wasiokuwa na hatia. Suala muhimu ni kwamba, utawala wa Kizayuni, licha ya kaulimbiu zake za awali na kujigamba kuhusu kuangamiza Hamas na hata kuwafukuza wakazi wote wa Gaza, bado haujafikia malengo hayo, na umeshindwa hata kukomboa idadi kubwa ya mateka wa Kizayuni ambao wako mikononi mwa makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina.

Katika matukio ya hivi karibuni kuhusiana na jambo, viongozi wa Tel Aviv, hasa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, wanazungumzia azma yao ya kufanya mashambulizi ya upande zote dhidi ya mji wa Rafah ulioko kusini mwa Gaza na karibu na eneo la mpaka na Misri, na tayari wamefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya  mji huo. Hivi karibuni Netanyahu alitangaza kwamba mashambulizi ya nchi kavu katika eneo hilo yataanza katika kipindi cha wiki mbili zijazo. Katika kuendeleza propaganda zake, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, ametoa wito wa kuangamizwa harakati ya Hamas huko Rafah kabla ya mwezi wa Ramadhani. 

Hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni imekabiliwa na upinzani mkubwa  wa walimwengu na hata washirika wake wa Magharibi, na maonyo mengi yametolewa kuhusu matokeo mabaya ya hujuma ya kinyama kama hiyo. Viongozi wa ngazi za juu wa Ufaransa na Uholanzi wameuonya utawala wa Kizayuni kuhusiana na jambo hilo.Hii ni pamoja na kuwa, mahakama za kimataifa pia zimepinga vikali jambo hilo. Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu uwezekano wa kushambuliwa mji wa Rafah na kusema kwamba mahakama hiyo itatawawajibisha wavunjaji wa sheria za kimataifa. Jumatatu iliyopita Karim Khan aliandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Nina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za uwezekano wa mashambuliwa ya nchi kavu ya Isreal huko Rafah. Ofisi yangu inafuatilia kwa karibu sana uhalifu wowote utakaofanyika katika uwanja huo, na yoyote atakayekiuka sheria atawafuatiliwa." Licha ya hayo, inaonekana kuwa kufeli kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kadhia ya Gaza na kutokuwepo utaratibu athirifu wa kimataifa wa kuilazimisha Israel ikomeshe mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu wa Gaza kwa uungaji mkono na himaya ya kisiasa na kijeshi wa Marekani, vimeushajiisha utawala huo kutekeleza mipango yake kuhusu Gaza, ikiwa ni pamoja na kufanya mashambulizi dhidi ya mji wa Rafah ambayo yatasababisha maafa makubwa na yasiyo na kifani ya binadamu kutokana na msongamano mkubwa wa watu katika eneo hilo. Utawala wa Kizayuni wa Israel unatekeleza jinai na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza kwa himaya ya nchi za Magharibi hususan Marekani, na hauzingati hata kidogo matakwa ya walimwengu ya kusitishwa mashambulizi yasiyokuwa na kikomo dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia yoyote wa Palestina.

342/