Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

19 Februari 2024

19:19:00
1439076

Kuzinduliwa mifumo mipya ya makombora nchini Iran

Katika kuendelea ustawi wa Jamhuri ya Kiislamu katika sekta ya makombora, mifumo dhidi ya makombora ya balestiki kwa jina la "Arman", na mfumo wa ulinzi wa anga ya juu wa Azarkhash, ambao uliundwa kwa juhudi za wataalamu wa Wizara ya Ulinzi ya Iran ulizinduliwa juzi Jumamosi.

Baada ya kutayarishwa, mifumo hii ya kutungua makombora inaweza kulenga na kuharibu shabaha husika katika muda wa chini ya dakika 3. Uwezo wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu utaongezeka kwa kiasi kikubwa kwa kuwepo mifumo hii mipya  ya kukabiliana na makombora katika mtandao wa ulinzi wa Iran.  

Makombora yaliyotumiwa katika mifumo ya kutungua makombora ya balestiki kwa jina la "Arman" wa aina ya Sayad-3 yana uwezo wa kukabiliana kwa wakati mmoja dhidi ya shabaha 6 katika umbali wa kilomita 120 hadi 180. Mfumo wa Azarakhsh ni mfumo wa kuwekwa kwenye majabari na wa masafa mafupi ambao kwa wakati mmoja hutumia rada na mfumo wa macho ya elektro-optiki  kwa ajili ya kutambua na kufuatilia shabaha.Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa mifumo mipya ya kutungua makombora katika mtandao wa ulinzi wa anga wa nchi, Brigedia Jenerali Amir Ashtiani Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema wizara yake imeelekeza nguvu zake zote katika kukidhi mahitaji ya uwanja wa ulinzi, zana na silaha za vikosi vya jeshi sambamba na uwezo wa ulinzi na muendelezo wa uzinduzi wa yaliyoahidiwa.

Wiki iliyopita, kwa mara ya kwanza, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilifanikiwa kurusha makombora ya balestiki yenye uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 1,700 kutoka katika meli ya kivita ya kikosi ch ulinzi kuelekea shabaha zilizowekwa. Mafanikio haya mapya yanamaanisha kuwa ushawishi na nguvu za kijeshi za majini na za makombora za Iran zitaongezeka na kufika hadi sehemu yoyote duniani kwa ajili ya kudhamini usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Maendeleo ya Iran katika sekta za makombora, mifumo ya ulinzi wa angani na ndege zisizo na rubani (droni) daima yamekuwa mwiba kwa maadui wa mfumo wa Kiislamu katika miaka ya hivi karibuni. Kuhusiana na nukta hii, kumekuwepo na utendaji kazi wa karibu na ushirikiano mkubwa kati Wizara ya Ulinzi ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC); na jambo hilo lina nafasi muhimu katika maendeleo ya sekta tajwa.



342/