Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

19 Februari 2024

19:19:32
1439077

Medvedev atishia kushambulia Washington, London na Berlin ikiwa Russia italazimishwa kuondoka Ukraine

Rais wa zamani wa Russia Dmitry Medvedev ametishia Washington, Berlin, London na Kiev kushambuliwa kwa silaha za nyuklia ikiwa Russia italazimishwa kujiondoa Ukraine.

Medvedev, ambaye ni Naibu Katibu wa Baraza la Usalama la Russia na mshirika wa karibu wa Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin ameandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba ikiwa Moscow italazimishwa kuachia eneo la Ukraine ambalo inalidhibiti, "haitasita" kufanya "maamuzi magumu".


Amefafanua kwa kusema: "majaribio ya kurejesha mipaka ya Russia ya 1991 itasababisha jambo moja tu - vita vya kimataifa na nchi za Magharibi kwa matumizi ya silaha zetu za kimkakati (nyuklia) dhidi ya Kiev, Berlin, London, na Washington na dhidi ya maeneo mengine yote mazuri ya kihistoria ambayo yamejumuishwa kwa muda mrefu kulengwa na ndege zetu kupitia mihimili ya pande tatu ya nyuklia".

Medvedev amesisitiza kuwa Russia ina "uthubutu wa kutosha" wa kuchukua hatua ikiwa nchi hiyo "itakaribia kutoweka."Rais huyo wa zamani wa Russia ameendelea kueleza katika ujumbe wake huo kwamba: "ni bora kurejeshwa kila kitu kabla muda kumalizika. Au tutairudisha sisi wenyewe na kusababisha hasara kubwa kwa adui kama ilivyotokea katika Avdiivka". Mwishoni mwa juma, vikosi vya Ukraine vililazimika kuondoka katika mji wa mashariki wa Avdiivka baada ya vita vya mwaka mzima. Mapema mwezi huu, Medvedev aliwakosoa washirika wa shirika la kijeshi la NATO kwa kile alichokiita "upayukaji hatari" juu ya uwezekano wa kutokea vita vikubwa baina yao na Russia. Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa X, Naibu Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia alisema: "jibu litakuwa si la mlingano ili kutetea umoja wa eneo la nchi yetu. Makombora ya balestiki na ya kruzi yanayobeba vichwa maalumu yatatumika.Hiyo inatokana na mfumo wetu wa kijeshi na kiulinzi ambao unajulikana na wote. Na huo utakuwa ndio mwisho wa kila kitu”.../   

342/