Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

19 Februari 2024

19:20:07
1439078

ICJ yaanza kusikiliza shauri la kihistoria kuhusu uhalali wa Israel kukalia ardhi za Palestina kwa miaka 57

Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ambayo ndiyo mahakama ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa leo imeanza kusikiliza shauri la kihistoria la kuamua kuhusu uhalali wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wa kuzivamia na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina kwa muda wa miaka 57.

Kesi hiyo itasikilizwa kwa muda wa wiki moja huko The Hague wakati utawala wa Kizayuni wa Israel ukiwa unaendeleza vita vya kikatili na mauaji ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Tangu viliponza Oktoba 7, 2023, vita na mauaji hayo ya kimbari yanayofanywa na jeshi la Kizayuni, yameshateketeza roho za Wapalestina zaidi ya 29,000.

Kesi hiyo ya kuchunguza uhalali wa Israel kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina kwa muda wa miaka 57 ni tofauti na ile ya mashtaka ya mauaji ya kimbari ambayo Afrika Kusini iliwasilisha katika mahakama hiyo ya ICJ dhidi ya utawala huo wa Kizayuni.

Badala yake, kesi hiyo iliyoanza leo inaangazia ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel katika Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na Quds Mashariki tangu mwaka1967.Wapalestina wanayataka maeneo yao yote hayo matatu kwa ajili ya kuunda nchi yao huru. Kwa mujibu wa timu ya wanasheria wa Palestina, wawakilishi wa Palestina, ambao wanatazamiwa kuzungumza leo Jumatatu, watajenga hoja kwamba uvamizi wa Israel ni kinyume cha sheria kwa sababu umekiuka kanuni tatu muhimu za sheria za kimataifa. Baada ya Wapalestina kuwasilisha hoja zao, katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa, zaidi ya nchi 50 na mashirika matatu ambayo ni Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Umoja wa Afrika zitahutubia majaji wa ICJ katika ukumbi mkuu wa mahakama hiyo. Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kupitisha Desemba 2022 kwa wingi mkubwa wa kura uamuzi wa kuliuliza na kulitaka jopo la majaji 15 wa ICJ litoe maoni ya ushauri kuhusiana na uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel. Hii ni mara ya pili kwa Baraza Kuu la UN kuitaka ICJ, ambayo pia inajulikana kama Mahakama ya Dunia, itoe maoni ya ushauri kuhusiana na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Mnamo Julai 2004, mahakama hiyo ilitamka kuwa ukuta wa kizuizi uliojengwa na utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi umekiuka sheria za kimataifa na unapaswa kuvunjwa, ingawa Israel haikujali uamuzi huo na ukuta huo ungali ungalipo hadi sasa.../

342/