Main Title

source : Parstoday
Jumatano

21 Februari 2024

12:47:31
1439466

Matukio ya Magharibi mwa Asia; ajenda kuu ya mazungumzo ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Saudi Arabia

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia wamejadili kuhusu matukio ya kieneo na kimataifa, vikiwemo vita vya Gaza na kuimarisha uhusiano wa simu.

Tangu kufikiwa makubaliano mwezi Machi mwaka jana (2023) kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia kwa upatanishi wa China, viongozi wakuu wa Tehran na Riyadh wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala yenye maslahi hususan matukio ya kieneo kupitia mashauriano mengi.

Katika mazungumzo ya simu hivi karibuni, Hussein Amir-Abdollahian na Faisal bin Farhan bin Abdullah, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia walijadili uhusiano wa pande mbili kati ya Tehran na Riyadh na kubadilishana mawazo kuhusiana na matukio ya kieneo na kimataifa, ikiwa ni pamoja na matukio ya hivi karibuni katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza, hali ya kibinadamu katika eneo hili na juhudi zilizofanywa katika uwanja huu.Tangu kuanza kwa mashambulizi na hujuma ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, Iran na Saudi Arabia mara kadhaa zimeeleza wasiwasi zilionao kuhusu kuendelea jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina na ulazima wa kukomesha jinai hizo za utawala vamizi wa Israel, kuondolewa mzingiro wa kibinadamu na kurejesha amani katika eneo hilo.

Saudi Arabia ambayo ilikuwa imekubali kuanza mchakato wa kurejesha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kabla ya tarehe 7 Oktoba 2023, ilitangaza kuwa imesimamisha mazungumzo yoyote kuhusiana na suala hilo baada ya kushadidi mashambulizi dhidi ya ardhi za Palestina. Hatua hiyo ilikaribishwa na Iran.

Hivi sasa Tehran na Riyadh zikiwa ni madola mawili yenye taathira katika matukio ya eneo huku zikitilia mkazo na kujaribu kusimamisha vita huko Gaza zinataka kushadidishwa mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni na kuongezwa misaada kwa wakaazi wapatao milioni mbili walioathiriwa na vita wa Gaza.

Kuhusu matukio ya Gaza, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa mauaji ya halaiki yanayotokea katika eneo hilo yanatokana na idhini na uungaji mkono kamili wa Marekani, na taathira mbaya za kuendelea mauaji ya Kizayuni katika usalama na uthabiti wa eneo ni jambo lisiloepukika.Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inaona kuna ulazima wa kufanyika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuhusu Gaza, na Saudi Arabia pia inaunga mkono suala hilo.

Mbali na kadhia ya Gaza na kutilia mkazo kuzidisha uhusiano kati ya Tehran na Riyadh katika sekta mbalimbali, jambo lingine muhimu la mazungumzo kati ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Saudi Arabia lilikuwa ni suala la kushiriki Wairani katika ibada ya Umra ambalo Faisal bin Farhan alisisitiza kuwa, kuhusu suala hilo hakuna matashi ya kisiasa katika Umrah, na utatuzi wa masuala ya kiufundi katika Shirika la Ndege la Saudia upo katika hatua zake za mwisho.

Faisal bin Farhan alielezea matumaini ya kuanzishwa tena safari za Umra kwa mahujaji wa Iran kwenda Makka na Madina katika siku za usoni.

Safari za Umra za mahujaji wa Iran zilitakiwa kuanza Januari 3 ya mwezi uliopita wa Januari baada ya kusimama kwa takriban miaka minane, ambapo hadi sasa safari hizo zimesitishwa kutokana na kutotolewa kwa vibali vya ndege za Iran.Mazungumzo chanya kati ya maafisa wakuu wa Iran na Saudi Arabia, hususan wakuu wa vyombo vya kidiplomasia vya nchi hizo mbili, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, yote yanaashiria kuwa, Iran na Saudi Arabia, kwa kuelewa hali nyeti ya eneo, zina shauku na hamu ya kupiga hatua na kusonga mbele katika kuimarisha mahusiano, na zinaamini kwamba, ufufuaji wa mahusiano haya upo katika uwezo wa nchi mbili hizo. Hii ni pamoja na kuwa, baada ya makubaliano ya Beijing kati ya Tehran na Riyadh, baadhi ya nchi za Kiarabu zilichukua hatua za kurejesha uhusiano na baadhi ya nchi nyingine pia zilichukua hatua za kuendeleza uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kufadhilisha kushirikiana na Riyadh na Tehran katika kukuza uhusiano huo badala ya migogoro, mivutano na mizozo. Ni dhahir shahir kwamba, kuboreshwa uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia yakiwa madola mawili makubwa ya mafuta na pia nchi mbili muhimu za Kiislamu, sanjari na kuanzisha ushirikiano mpya wa kisiasa na kiuchumi baina yao, hayo yatapelekea kuchukua wigo mpana uthabiti na usalama katika eneo hili na hivyo kupiga jeki utatuzi wa mizozo katika nchi kama vile Syria na Yemen.



342/