Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

23 Februari 2024

16:28:21
1439819

Iran: Kusimamisha vita na kuandaliwa kura ya maoni ndio suluhisho la kadhia ya Palestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa kusitishwa vita katika ukanda wa Gaza na kuandaliwa kura ya maoni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ndio njia pekee ya kupatikana amani katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran, IRNA, Nasser Kanani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, aliandika siku ya Alhamisi katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa "X" kwamba  misimamo na maamuzi ya hivi karibuni yaliyotangazwa na baraza la mawaziri la utawala bandia wa Israel na bunge la utawala huo wa Kizayuni ya kupinga kuundwa taifa huru la Palestina kwa mara nyingine tena ilifichua kwa uwazi utambulisho wa  utawala ambao ni utambulisho wa kivita na kukalia kwa mabavu ardhi za wengine.

Kanani Chafi ameongeza kuwa: "Mtazamo potofu wa utawala wa Kizayuni ni kukariri madai ya uongo kuhusu amani na mapatano yasiyo na tija ya huko nyuma. Kwa miongo kadhaa watawala wa Kizayuni wamekuwa wakitumia hila na hadaa katika mapatano."

Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran amesema: "Utawala wa Kizayuni unatumia ujanja kukanusha na kupuuza haki zisizopingika  za wananchi wa Palestina, ikiwa ni pamoja na haki ya kujitawala na kuunda taifa huru la Palestina katika ardhi zote za historia za Palestina."

Kanani Chafi ameongeza kuwa: "Taifa na wanamapambano (wanamuqawama) wa Palestina, kwa utambuzi na mwamko kuhusu malengo maovu ya Wazayuni, wanachukulia suluhisho pekee na la msingi la uvamizi wa Palestina kuwa ni kutumizwa irada ya taifa la Palestina ya kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu (Jerusalem).

Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi na mataifa mengine yanayopenda uhuru na yanayotafuta haki pia yanaunga mkono matakwa na haki za wananchi wa Palestina ambazo zimepuuzwa kwa zaidi ya miongo 7.

Amesisitiza kuwa: "Njia pekee ya kumaliza vita na umwagaji damu na kurudisha amani na usalama katika eneo ni kuheshimu kura za wananchi wote wa Palestina kwa kuandaa kura ya maoni ili kutekeleza haki ya kujitawal ya wakazi wa asili wa Palestina.