Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

24 Februari 2024

14:31:13
1440083

Idadi ya wagombea katika uchaguzi wa Bunge nchini Iran yaweka rekodi mpya tangu 1979

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran inaonesha kuwa, idadi ya watu waliojiandikisha kugombea viti vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) imevunja rekodi ya ile iyosajiliwa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mwaka 1979.

Taarifa hiyo inasema, wagombea 15,200 wameidhinishwa na vyombo husika kuwania viti 290 vya Bunge, idadi ambayo inaweka rekodi mpya tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, Ahmad Vahidi, amesema uwanja umeandaliwa kwa ajili ya ushindani halisi kati ya makundi yenye mielekeo tofauti ya kisiasa.

Amesema wagombea na wafuasi wao wanapaswa kuzingatia taratibu za kisheria za uchaguzi, akiwataka kufanya kampeni kwa nidhamu kamili na kuacha kuwadhalilisha wagombea wengine.Orodha ya wagombea waliotimiza masharti inajumuisha majina ya wanawake 1,713, ambayo ni zaidi ya mara mbili ya 819 waliogombe viti vya Bunge hapa nchini mwaka 2020. Kampeni za wagombea zaidi ya 15,000 wanaowania viti vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, zilianza rasmi Alkhamisi wiki hii. Msemaji wa Tume ya Uchaguzi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran amesema: " Kampeni za uchaguzi wa Bunge la 12 zilianza rasmi saa saba usiku wa kuamkia leo Alkhamisi na zitaendelea hadi saa mbili asubuhi ya tarehe 29 Februari". Mohsen Eslami ameongeza kuwa: Vituo 59,000 vya kupigia kura vimetengwa kote nchini Iran kwa ajili ya uchaguzi huo wa Bunge, na mawakala 800,000 wa Tume ya Uchaguzi wakiwemo wa asili na wa akiba wako tayari kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo. Uchaguzi wa 12 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa sita wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu utafanyika tarehe Mosi ya mwezi ujao wa Machi.

342/