Main Title

source : Parstoday
Jumapili

25 Februari 2024

16:24:18
1440257

Iran: Mataifa ya Kiislamu yachukue hatua za kuwanga mkono watu wa Gaza

Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran amesema mataifa yote ya Kiislamu yana wajibu wa kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kuwapa usaidizi wa kivitendo ili kuwafanya waondokane na hali mbaya ya kibinadamu inayowakabili.

Mohammad Mehdi Esmaili amesema hayo katika mkutano wake na Abdulrahman bin Hamad bin Jassim bin Hamad Al Thani, Waziri wa Utamaduni wa Qatar, ambapo amepongeza mchango na uungaji mkono wa Doha kwa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa kwa kupitia vyombo vya habari.

Esmaili ameeleza bayana kuwa, "Tunapaswa kujaribu kuziasa nchi zote za Kiislamu kufanya kila ziwezalo kuwaunga mkono watu wa Gaza na kuchukua hatua za kivitendo za kuwaondolea Wapalestina hao machungu wanayoyapitia."

Aidha Waziri wa Utamaduni wa Iran ametoa mwito wa kubuniwa mkakati maalumu katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), utakaonakili jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.Alitoa mwito huo jana Jumamosi huko Istanbul, Uturuki katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Habari na Utamaduni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) cha kujadili hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza. Waziri huyo wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran amesema ukusanyaji wa ushahidi madhubuti unaweza kusaidia kuwajibishwa na kubebeshwa dhima Israel kwa jinai na vitendo vyakevisivyo vya kiutu dhidi ya Wapalestina. Esmaili amebainisha kuwa, Iran inatoa mwito wa kuimarisha ushirikiano wa vyombo vya habari miongoni mwa nchi wanachama wa OIC, kama sehemu ya kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza.

342/