Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

26 Februari 2024

19:24:25
1440570

Kan'ani: Marekani na Uingereza zinatoa kafara usalama wa kimataifa kwa maslahi ya Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amelaani vikali mashambulizi mapya ya anga ya "kiholela" yaliyofanywa na Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen, akisema hujuma hiyo imethibitisha kwa mara nyingine kwamba nchi hizo mbili zinatoa kafara usalama wa kimataifa kwa maslahi ya Israel.

Nasser Kan’ani aliyasema hayo jana Jumapili baada ya vikosi vya Marekani na Uingereza kufanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen, ukiwemo mji mkuu, Sana’a.

"Mashambulizi hayo ya kiholela na ya kidhalimu yanakiuka sheria na kanuni zinazotambulika kimataifa na yanakiuka mamlaka na kujitawala ya Yemen," alisema Nasser Kan'ani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa: "Marekani na Uingereza kwa mara nyingine tena zimethibitisha kwamba zinaunga mkono kikamilifu jinai za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel na mauaji ya kimbari yanayofanyika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kwamba zinatangulizia mbele usalama na maslahi haramu ya utawala huo ghasibu kuliko amani na usalama wa kimataifa."

Katika taarifa yake, Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imedai kuwa mashambulizi hayo yamefanywa kwa msaada wa Australia, Bahrain, Canada, Denmark, Uholanzi na New Zealand kwa nia ya "kudhoofisha" uwezo wa Yemen wa kufanya mashambulizi ya baharini ya kuwatetea na kuwaunga mkono Wapalestina. 

Kan’ani amesema kuwa Marekani na Uingereza zimeonesha kuwa zinakiuka kanuni zote za kimaadili na za kibinadamu, pamoja na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Badala ya kuchukua hatua madhubuti na za haraka kuondoa sababu kuu ya ukosefu wa usalama na utulivu, ambayo ni mashambulizi na uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na mauaji yake ya kila siku ya mamia ya Wapalestina ..., Marekani na Uingereza zinafanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi ambayo inajaribu kuuwekea mashinikizo utawala katili na kusimamisha mashine yake ya kuua watu."

342/