Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

29 Februari 2024

20:58:24
1441301

Safari za ndege baina ya Iran na Oman zaongezeka maradufu, biashara yazidi kustawi

Wakuu wa mashirika ya ndege ya Iran na Oman wamesema kuwa, safari za ndege baina ya nchi hizi mbili ndugu za Kisilamu zimeongezeka maradufu hivi sasa kutoka safari 30 hadi 60 kwa wiki.

Hayo yameelezwa kwenye mazungumzo baina ya Mkuu wa Shirika la Anga la Oman, Naif Ali al Abri na Mohammad Mohammadi Bakhsh, Mkuu wa Shirika la Anga la Iran. Mkutano huo umeshuhudia kutiwa saini hati ya ushirikiano zaidi baina ya pande mbili katika masuala ya usafiri na uchukuzi.

Huku hayo yakiripotiwa, Waziri wa Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii wa Iran ameonana na Waziri wa Kazi wa Oman na pande mbili zimetilia mkazo wajibu wa kustawishwa zaidi ushirikiano baina ya Tehran na Muscat katika nyuga tofauti. Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Sayyid Sowlat Mortazavi, Waziri wa Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii wa Iran ameonana na Waziri wa Kazi wa Oman, Mahad bin Said bin Ali Baawain na pande mbili zimesisitizia wajibu wa kutanuliwa wigo wa ushirikiano wa pande mbili kwenye nyuga nyingi zaidi na kwa upana zaidi.

Mwaka uliopita, mabadilishano ya kibiashara baina ya pande hizi mbili yaliongezeka kwa asilimia 42 na nafasi ya kutosha ipo kwa ajili ya kuongeza kiwango cha mabadilishano hayo na kukifikisha kwenye dola bilioni 4 kwa mwaka.

Kwa upande wake, Balozi wa Oman nchini Iran, Ibrahim Ahmad Mohamed Al-Muaini amesema kuwa, kuna makubaliano makubwa baina ya Tehran na Muscat yanayohusiana na ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya nchi hizi mbili.