Main Title

source : Parstoday
Jumapili

3 Machi 2024

18:15:01
1441953

Raisi: Iran ipo tayari kuipa Msumbiji uzoefu wa kiufundi na kiuhandisi

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ina hamu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na mataifa ya Afrika ikiwemo Msumbiji na kuongeza kuwa, kuna haja ya kubuni ramani mpya ya njia na kuamilisha Kamisheni ya Pamoja ya Iran na Msumbiji ili kupiga jeki ushirikiano wa pande mbili.

Sayyid Raisi amesema hayo katika mkutano wake na Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, pambizoni mwa Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi Zinazouza Gesi Duniani (GECF) nchini Algeria na kuongeza kuwa, Iran ipo tayari kuipa Msumbiji huduma za kiufundi na kiuhandisi.

"Mkutano huu unaweza kufungua ukurasa mpya katika muelekeo wa kuimarisha na kuboresha ushirikiano baina ya nchi mbili," ameeleza Rais Raisi.

Rais wa Iran amebainisha kuwa, utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi kwa kuunga mkono ugaidi, zinaziweka nchi za Afrika chini ya mashinikizo na kupora rasilimali zao. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kushirikiana na Afrika katika vita dhidi ya ugaidi.

Kwa upande wake, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amesema nchi yake inatazama suala la kuimarisha uhusiano na Iran kuwa msingi wa kufikia malengo muhimu, huku akitoa mwito wa kutekelezwa makubaliano baina ya nchi mbili hizi.