Main Title

source : Parstoday
Jumapili

3 Machi 2024

18:16:04
1441954

Mamia waandamana nje ya ubalozi wa Israel, Washington kulaani vita Gaza

Mamia ya watu wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington, Marekani kulaani vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Waandamanaji hao walikusanyika mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington, sehemu aliposimama Aaron Bushnell, afisa wa Jeshi la Anga la Marekani, ambaye alifariki dunia hivi karibuni baada ya kujichoma moto akipinga uungaji mkono wa nchi yake kwa vita vya mauaji ya kimbari vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Mmoja wa waandamanaji hao amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, "Ujumbe mkuu kwenye mkusanyiko huu ni Palestina Huru. Hicho ndicho kitu ambacho kila mmoja anakitaka."

Bushnell ambaye alikuwa na umri wa miaka 25, alisikika akisema "Palestina Huru" wakati akijichoma moto mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington D.C, katika tukio hilo la Jumapili iliyopita, ambalo limeendelea kuishangaza dunia nzima.Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanani hao mjini Washington yalikuwa na jumbe zinazosema: Israel inatekeleza sera ya kuwaangamiza wananchi wa Palestina; ukatili basi, na unyanyasaji basi.

Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Kuunga Mkono Watu wa Palestina yalifanyika katika nchi mbali mbali kote duniani Jumamosi ya jana, kuanzia Marekani, Cuba, Bolivia, nchi za Kiarabu na hata katika nchi nyingi za Ulaya.

Walimwengu wanaendelea kueleza hasira na upinzani wao dhidi ya mashambulizi na mauaji ya watu wasio na hatia huko Gaza huku nchi za Magharibi zikiendelea kuunga mkono utawala wa Kizayuni, ambapo mpaka sasa umeua shahidi Wapalestina zaidi ya 30,000.