Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

4 Machi 2024

19:56:40
1442204

Iran: Juhudi za serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ni kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na Afrika

Naibu Waziri wa wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya uchumi amesema kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje na balozi za Iran nje ya nchi zinafuatilia kwa dhati maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi na nchi za bara la Afrika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars; Mehdi Safari amesema hayo wakati alipofanya mkutano kwa njia ya video na mabalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran barani Afrika na kusisitiza kuwa, serikali ya 13 Jamhuri ya Kiislamu chini ya urais wa Rais Ebrahim Raisi inalipa kipaumbele kikubwa suala la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi za Afrika na ni jukumu la wawakilishi wa Iran nje ya nchi kutumia hadhi zao za kidiplomasia kusaidia kuimarisha mahusiano ya kibiashara baina ya Iran na bara hilo.

Ameongeza kuwa, bidhaa zisizo za mafuta hasa katika sekta ya elimu, dawa na vifaa tiba na huduma za kisayansi na kiteknolojia sambamba na bidhaa za chakula na zana mbalimbali, vifaa vya ujenzi na huduma za kiufundi na uhandisi, zina uwezo mkubwa wa kukuza mauzo ya bidhaa za Iran barani Afrika.

Naibu Waziri wa wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya uchumi vilevile ameashiria ulazima wa kusahihishwa mitazamo kuhusu bara la Afrika na kuzingatia fursa nyingi na tofauti zinazopatikana katika bara hilo kwa ajili ya kukuza uchumi wa Iran katika nyuga mbalimbali zikiwemo mauzo ya bidhaa za Irana na ushirikiano katika nyanja ya kutoa mafunzo ya kiufundi na kitaaluma.

Ameongeza kuwa: Wizara ya Mambo ya Nje na balozi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinafuatilia kwa dhati maendeleo ya pande zote za ushirikiano wa kiuchumi na nchi za Afrika ili kusaidia wanaharakati wa kiuchumi na makampuni yenye uwezo wa kusafirisha bidhaa na kutoa huduma za kiufundi na kiuhandisi.

342/