Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

4 Machi 2024

19:57:11
1442205

Raisi: Chimbuko la jinai za Wazayuni Ghaza linarejea kwenye miaka 75 ya uvamizi wao

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kinachojiri leo Ghaza ni mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita, na chimbuko la jinai hiyo linarejea kwenye historia ya miaka 75 ya uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Wazayuni.

Kwa mujibu wa IRNA, Rais Raisi, amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Algiers aliofanya pamoja na mwenyeji wake Rais Abdel Majid Taboun wa Algeria, ambapo sambamba na kuipongeza serikali ya nchi hiyo kwa kuendesha kwa mafanikio Mkutano wa saba wa Baraza la Viongozi wa Nchi Zinazouza Gesi kwa wingi duniani, amesema uhusiano wa Iran na Algeria unakwenda mbali zaidi ya uhusiano wa kisiasa kwa sababu unatokana na mafungamano ya karibu mno katika nyuga za dini, utamaduni na ustaarabu. Rais wa Iran amewaenzi pia mashahidi wa mapambano ya Algeria dhidi ya ukoloni na akasema: "tunawaheshimu Mujahidina wote waliouawa shahidi, ambao walisimama dhidi ya wakoloni kwa istiqama na uvumilivu na uaminifu kwa Uislamu na nchi, na tunaziombea amani roho zao safi".Sayyid Ebrahim Raisi amegusia misimamo ya pamoja ya kisiasa ya Iran na Algeria hususan katika kutetea haki za wananchi madhulumu wa Palestina na kupinga jinai na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala wa Kizayuni na akasema: kinachojiri leo Ghaza ni mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita, na chimbuko la jinai hiyo linarejea kwenye historia ya miaka 75 ya uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Wazayuni.

 Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea pia masikitiko yake makubwa juu ya kuendelea uhusiano kati ya baadhi ya nchi za Kiislamu na utawala wa Kizayuni, licha ya kuendelea vitendo vya jinai unavyofanya utawala huo dhidi ya wananchi madhulumu wa Ghaza, na akasema: kuvunja uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na utawala huo ni miongoni mwa mambo yatakayoweza kuzuia uhalifu na jinai unazofanya. Raisi amesisitiza pia kuwa: "kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina ni moja ya misingi isiyobadilika ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sisi hatujawahi katu kusitasita katika kuunga mkono haki za wananchi wa Palestina, na tunaamini kuwa njia itakayohakikisha Wapalestina wanapata haki zao ni kura za watu wa Palestina wakiwemo Waislamu, Wakristo na Wayahudi." Aidha ameashiria mazungumzo yaliyofanyika katika kikao cha jumbe za ngazi za juu za nchi mbili na akasema: viongozi wakuu wa Iran na Algeria wameazimia kustawisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara sambamba na kustawisha uhusiano wa kisiasa na uwezo mkubwa sana zilionao nchi mbili unaandaa mazingira mwafaka ya kuinua kiwango cha mahusiano ya kiuchumi.../