Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

7 Machi 2024

14:14:05
1442837

Kiongozi Mkuu: Mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya kusimama imara kukabiliana na kambi ya Uistikbari

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema, mantiki ya kidini, kiakili na ya kiutu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya kusimama imara kukabiliana na kambi ya Uistikbari.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano na Mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu.Akibainisha mantiki hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kusimama imara na kukabiliana na watumiaji mabavu, Ayatullah Khamenei amesema: hadi kabla ya kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu, kambi pekee iliyokuwepo duniani ilikuwa ni ya demokrasia zenye mfungamano na demokrasia ya kiliberali ya Magharibi, lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, iliundwa kambi mpya ya mfumo wa Kiislamu unaoendana na ridhaa ya wananchi, ambayo kimsingi ulisimama kukabiliana na demokrasia ya Magharibi.Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kujitokeza kwa kigezo cha Mfumo wa Kiislamu unaotokana na ridhaa ya wananchi nchini Iran kulihatarisha maslahi ya kambi ya demokrasia ya Magharibi na kuanza mizozo na upinzani wa kila mara wa mfumo huo dhidi ya Mfumo wa Kiislamu na akaongezea kwa kusema: sababu ya wao kuhisi hatari hiyo na kuanzisha upinzani wao ni kwamba katika dhati ya mfumo wa demokrasia ya Magharibi kuna hulka ya kiburi, uchokozi, uporaji wa haki za mataifa na kuzusha vita na umwagaji damu usio na kikomo ili kunyakua madaraka; na ushahidi wa hayo ni kukoloniwa nchi nyingi za Asia, Afrika na Amerika ya Kusini katika karne ya 19, yaani, wakati wa kilele cha kauli mbiu na madai yao ya demokrasia, uhuru na haki za binadamu.Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, dhati ya Kiislamu ndilo suala muhimu zaidi na muelekeo wa kambi ya Mfumo wa Kiislamu unaotokana na ridhaa ya wananchi katika kukabiliana na dhulma na uonevu huo; na katika kujibu suali la kwa nini Jamhuri ya Kiislamu inakabiliana na kambi ya Uistikbari amesema: Iran ya Kiislamu haina ugomvi wowote na nchi, serikali na mataifa, bali inapinga dhulma na uchokozi uliomo ndani ya kambi ya demokrasia ya Magharibi.

Ayatullah Khamenei ameyataja matukio ya kusikitisha ya huko Ghaza kuwa ni mfano wa wazi wa dhulma na uchokozi wa kambi ya Uistikbari dhidi ya wamiliki halisi wa ardhi, mauaji ya kikatili na kinyama ya wanawake na watoto na uharibifu wa mali na rasilimali za watu wa ardhi hiyo na akasema: upinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa hakika ni wa kupinga ukatili huo na jinai ambazo licha ya kulaaniwa na kila akili, hukumu ya dini na dhamiri za wanadamu zinaungwa mkono na Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi za Ulaya.Amesisitiza kuwa: ni lazima ibainishwe na kujulikana wazi kwamba kambi ya Uistikbari imeficha dhulma, uchokozi na mauaji chini ya jina la demokrasia, haki za binadamu na uliberali.Aidha, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kubainishwa mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kusimama imara na kukabiliana na Waistikbari kwa vizazi vipya ni jukumu moja muhimu na akaongeza kuwa: kwa bahati nzuri, katika kipindi cha zaidi ya miongo minne ya umri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imeonyeshwa kwa walimwengu sura halisi, kambi yenyewe na muelekeo wa kupambana na Uistikbari.../