Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

7 Machi 2024

14:15:04
1442839

Iran na Sierra Leone kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Sierra Leone wametilia mkazo wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa kiuchumi na kisiasa baina ya nchi zao.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la IRNA ambalo limemnukuu Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema katika mazungumzo yake na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Sierra Leone, Timothy Musa Kabba, kwamba kuna udharura wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa Tehran na Free Town kwenye nyuga zote hasa za kiuchumi na kisiasa.

Kadhia ya Palestina hasa vita vya Ghaza na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina ni maudhui nyingine iliyozungumziwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Sierra Leone kwenye mazungumzo yao hao yaliyofanyika pambizoni mwa kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, mjini Jeddah, Saudi Arabia.Sierra Leone ni mwanachama wa OIC ambayo hivi karibuni ililaani vikali jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza kwa miezi mitano sasa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alirejea humu nchini jana Jumatano baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku mbili mjini Jeddah, Saudi Arabia alikokwenda kuhudhuria kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC ambacho kimejaili kadhia ya Palestina hasa Ukanda wa Ghaza.

Katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametaka utawala wa Kizayuni wa Israel ususiwe kikamilifu, kimataifa na kwenye nyuga zote kutokana na jinai zake za kupindukia dhidi ya Wapalestina.