Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Machi 2024

19:46:13
1443262

Mwendesha Mashtaka wa ICC atuhumiwa kuonyesha undumilakuwili wa wazi kuhusiana na Ghaza

Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Med Human Rights Monitor (Euro-Med) limesema Karim Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ameonyesha "undumilakuwili" katika kukabiliana na uhalifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Ghaza.

Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Geneva limeeleza katika taarifa kwamba lina wasiwasi mkubwa kwamba ICC haiwezi kutekeleza majukumu yake na kwamba jambo hilo litasababisha madhara yasiyoweza kurejesheka kwa haki za watu wa Palestina. Taarifa ya Euro-Med imesisitiza kuwa, ICC inapaswa kuchukulia kwa uzito wa hali ya juu uhalifu wa mauaji ya kimbari uliofanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza. Shirika hilo la haki za binadamu limekumbusha kuwa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) tayari imeshathibitisha tuhuma kwamba mauaji ya kimbari yamefanywa na Israel katika ardhi hiyo ya Palestina iliyowekewa mzingiro. Taarifa hiyo ya Euro-Med imeeleza bayana kwamba, kuna tofauti za wazi katika jinsi kesi zinazowasilishwa kwa ICC zinavyoshughulikiwa, hasa inapolinganishwa utaratibu unaofuatwa kushughulikia kadhia na hali ya Palestina na mzozo wa Ukraine.Shirika la Euro-Med Monitor limesema jinai na uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel umekwenda mbali zaidi ya uharibifu wa miundombinu na mali za raia. Likifafanua zaidi, shirika hilo la kutetea haki za binaadamu limesema, "uhalifu huu umeharibu maisha ya wakazi wote wa Ukanda wa Ghaza, umewaangamiza kikamilifu Waghaza kupitia vitendo vya mauaji ya kimbari ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki na ya makusudi, kuwalenga kwa makusudi na kiholela raia wakiwemo maelfu ya wanawake na watoto, kuwadhikisha kwa njaa, kuwanyima vitu vya msingi, kuwahamisha kwa nguvu na kuwaacha bila makazi, kuwakatia maji na umeme, kuwakosesha huduma za matibabu, kuwawekea vizuizi haramu, kuwazuilia misaada ya kibinadamu, kuziteketeza athari zao za kiutamaduni, kihistoria na kidini pamoja na hospitali, ambavyo vyote hivyo havipasi kuwa walengwa wa hujuma za kijeshi kwa namna yoyote ile, kuwakamata watu kiholela, kuwafanya watoweke kwa kulazimishwa, kuwaandama kwa mateso, kuamiliana nao kikatili, kuwabaka, kupora mali zao na kutumia silaha zilizopigwa marufuku dhidi yao”.

342/