Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Machi 2024

19:47:25
1443264

HAMAS: Tume ya kimataifa isiyo na upendeleo ichunguze tuhuma za ukatili wa kingono wa Oktoba 7

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetaka "tume ya kimataifa ya uchunguzi isiyo na upendeleo" iundwe ili kuchunguza madai kwamba wapiganaji wake walihusika na ukatili wa kingono walipotekeleza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Oktoba 7, 2023.

Harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina imekanusha tuhuma zilizotolewa na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwamba wapiganaji wake waliwafanyia ukatili wa kingono wanawake Waisrael wakati wa shambulio hilo. Pramila Patten, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Ukatili wa Kingono katika Migogoro, alidai katika ripoti yake aliyotoa Jumatatu kwamba kuna "sababu za kuridhisha za kuamini" ukatili wa kingono, ikiwa ni pamoja na ubakaji na ubakaji wa halaiki, ulitokea wakati wa shambulio lililofanywa na Hamas. Basem Naim, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba Hamas haikubaliani na ripoti ya Patten na akabainisha kuwa ripoti hiyo imekuja baada ya Israel kushindwa kuthibitisha madai yoyote ya aina hiyo.Ikifafanua zaidi, Hamas imeendelea kueleza kwamba ripoti hiyo imetolewa baada ya kushindwa majaribio ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuthibitisha madai hayo bandia, ambayo yamethibitishwa kuwa hayana msingi wowote, yakilenga kuuchafua tu muqawama wa Palestina na kuhafifisha ripoti ya maripota wa Umoja wa Mataifa kuhusu ushahidi wa kutosha unaothibitisha ukiukaji wa kutisha wa haki za binadamu waliofanyiwa wanawake na wasichana wa Kipalestina na askari wa jeshi la utawala huo haramu. Aidha, Hamas imetilia mkazo nia yake ya kushirikiana kikamilifu na tume ya uchunguzi na kuheshimu matokeo yatakayotangazwa na tume hiyo. Kauli ya Hamas imekuja wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kukutana Jumatatu kujadili ripoti hiyo ya Patten. Hayo ni kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Times of Israel. Itakumbukwa kuwa, mnamo Februari 19, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakiwemo maripota maalumu wa umoja huo walieleza katika ripoti ya uchunguzi wao kwamba, mamia ya wanawake na wasichana wa Kipalestina katika maeneo ya Ghaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu wamekuwa wakiwekwa kizuizini kiholela na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel tangu Oktoba 7, na kuripoti kuwa wamebakwa, kupigwa vibaya na kunyimwa chakula na dawa na askari wa jeshi hilo.../

342/