Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Machi 2024

19:48:25
1443266

Tehran: Taasisi za haki za binadamu za UN ni ‘mwanasesere’ wa baadhi ya tawala za Magharibi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepinga ripoti ya ujumbe uliopewa mamlaka na Umoja wa Mataifa kuhusu machafuko ya 2022 nchini Iran, akisema kwamba mifumo ya haki za binadamu wa chombo hicho cha kimataifa imegeuka kuwa "mwanasesere" mikononi mwa baadhi ya tawala ili kuendeleza uovu wao.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumamosi, Nasser Kan’ani amepinga vikali yaliyomo katika ripoti hiyo iliyochapishwa  na Baraza la Haki za Kibinadamu la Baraza la Umoja wa Mataifa akisema ripoti hiyo imekariri madai yasiyo na msingi yaliyojikita katika taarifa zisizo sahihi na zenye upendeleo: hivyo haina uaminifu wa kisheria na haikubaliki.

Kan'ani amelaani majaribio ya kuchochea chuki dhidi ya Iran na akisema kuwa, kile kinachojulikana kama "ujumbe wa kutafuta ukweli" kilianzishwa na kufadhiliwa mnamo Novemba 2022 na serikali kadhaa za nchi za Magharibi, haswa Ujerumani, kama matokeo ya "maonyesho ya kipuuzi ya haki za binadamu".

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema ripoti ya ujumbe huo inakusanya upotoshaji uliopangwa na uongo ambao umebadili ukweli kimakusudi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitambua ripoti hiyo iliyotungwa na kutengenezwa na utawala wa Kizayuni, Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi kuwa ni mfano wa wazi wa matumizi mabaya ya dhana na maadili matukufu ya haki za binadamu kwa ajili ya malengo mafupi ya kisiasa. Inaamini kuwa ripoti hiyo haikubalika kisheria na haina athari yoyote."

Kan'ani amesisitiza kuwa ripoti hiyo imefichua kuwa kile kinachojulikana kama "ujumbe wa kutafuta ukweli" kinafanya kazi kwa kufuata njama za waanzilishi wake yaani Ujerumani, Uingereza, Marekani na Israel, na kutumia vibaya mifumo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kutimiza malengo maovu na haramu ya tawala hizo.

Katika ripoti hiyo, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulidai siku ya Ijumaa kwamba jibu la Iran kwa ghasia zilizozuka kufuatia kifo cha msichana wa Kiirani mnamo Septemba 2022 ni sawa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

342/