Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Machi 2024

19:49:20
1443268

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran: Tuitumie vyema fursa ya mwezi mtukufu wa Ramadhani

Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amewataka Waislamu kujiandaa vizuri kwa ajili ya kuingia kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani kama ambavyo pia amesisitiza kwamba, washindi wa vita vya utawala wa Kizayuni huko Ghaza, ni Wapalestina.

Katika kutba zake mbili zilizokusanya vitu vingi, Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami ameanza kwa kuzungumzia umuhimu mkubwa wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kunukuu hadithi ya Bwana Mtume Muhammad SAW inayopatikana kwenye jildi ya 96 ya Kitabu cha Hadith cha Bihar al Anwar ukurasa wa 340 ambapo Bwana Mtume anawahimiza Waislamu akiwaambia, msiuangalie mwezi wa Ramadhani kwa jicho sawa la miezi mingine ya mwaka kwani Mwenyezi Mungu ameupa fadhila kubwa sana mwezi huo. Ameendelea kunukuu hadith hiyo kwa kusema kuwa, ndani ya mwezi wa Ramadhani, Muislamu anatakiwa kuchunga zaidi ulimi wake na macho yake na masikio yake na kila kitendo chake kuliko anavyochunga kwenye miezi mingineyo ya mwaka kwani ndani ya mwezi huo anakuwa ni mgeni wa Allah na utukufu wa ugeni huo ni mkubwa sana.Katika sehemu nyingine ya khutba zake za Sala ya Ijumaa ya leo, Ayatullah Khatami amelaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza na kuongeza kuwa, vita hivyo vimefichua unyama na ukatili wa kuchupa mipaka wa Wazayuni na viongozi wa madola ya kibeberu ya Magharibi hasa Marekani, lakini jambo lisilo na shaka ni kwamba wananchi wa Palestina ndio watakaoshinda vita hivyo. Katika kipindi cha miezi mitano ya jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza, karibu Wapalestina 31,000 wameshauwa shahidi na zaidi ya 72,000 wameshajeruhiwa hadi hivi sasa, wengi wao ni wanawake na watoto wadogo.