Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

11 Machi 2024

14:42:43
1443699

Yemen yawaasa Waislamu wasusie bidhaa za Israel, Marekani

Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ametoa mwito kwa mataifa ya Kiislamu na Kiarabu kususia bidhaa zinazozalishwa na Israel na Marekani, akisisitiza kuwa hatua hiyo itakuwa ni zawadi ndogo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wanaoendelea kuuawa kikatili na utawala wa Kizayuni.

Shirika la habari la Al-Masirah limemnukuu Mahdi al-Mashat akisema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwa mnasaba wa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuongeza kuwa, kususia bidhaa za Isreal na waitifaki wake ni moja ya njia bora za kupaza sauti dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni. 

Amesema vita vya Gaza vimefichua sura halisi ya Marekani ambayo amekuwa ikijinadi kuwa kinara wa haki za binadamu duniani. Al-Mashat amebainisha kuwa, Marekani inaunga mkono mauaji ya halaiki, kwa kuuunga mkono utawala muuaji wa watoto wadogo na mkanyagaji wa haki za mataifa mengine.

"Mwezi mtukufu wa Ramadhani umewadia, na ndugu zetu wa Palestina hasa Gaza wanaendelea kuwajihiwa na mauaji ya kimbari ya Israel kwa miezi sita mfululizo," ameongeza al-Mashat.Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ameongeza kuwa, Marekani haikubali kabisa juhudi za kimataifa za kusimamisha vita Gaza, na ithibati ya hiyo ni namna Washington ilivyotumia kura yake ya veto mara tatu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupinga maazimio ya usitishaji vita na yaliyotaka pia kutumwa misaada ya kibinadamu Gaza.

Mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na mauaji ya kimbari ya watu wasio na hatia wa Palestina, yamepelekea kuendelea kususiwa zaidi bidhaa mashuhuri zinazozalishwa na mashirika ya utawala huo au makampuni yanayouunga mkono duniani.

Al-Mashat amengoeza, kuwa, vikosi vya Yemen vitaendeleza operesheni zake dhidi ya Israel na waitifaki wake katika eneo la Bahari Nyekundu hadi pale hujuma dhidi ya Ukanda wa Gaza zitakapokoma na mzingiro wa eneo hilo kuondolewa.   


\342