Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

11 Machi 2024

14:43:57
1443704

Muigizaji wa kimataifa Khaled Abdullah: Ramadhani itukumbushe njaa ya watu wa Gaza

Muigizaji wa Uingereza mwenye asili ya Misri, Khaled Abdullah, ametuma ujumbe wa kuwaunga mkono watu wa Palestina kupitia akaunti yake kwenye jukwaa la "X", akisema mwanzo wa mwezi wa Ramadhani ni fursa ya kukumbuka mateso ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kuwaokoa kutokana na njaa.

Muigizaji huyo wa Uingereza ameandika kuwa: Ni siku ya kwanza ya Ramadhani. Wakati huu #Gaza inapotumbukizwa kwenye njaa sijawahi kuhisi vyema zaidi kuliko sasa yale niliyoambiwa nikiwa mtoto kuhusu funga ya Mwezi wa Ramadhani; Ni kuelewa na kuhisi wanayopitia watu ambao hawakubahatika kuwa hali kama yako. 

Muigizaji Khaled Abdullah ameongeza kuwa: "Natarajia duniani kote mabilioni ya watu wanatumia Gaza kama mfano kuelezea funga ya #Ramadan kwa watoto wao. Siwezi kukuelezea jinsi hilo linavyoumiza."Tarehe 3 Machi, mwigizaji huyo, alitangaza kupitia akaunti yake ya Instagram kwamba amejiunga na kampeni ya kuchangia misaada ya matibabu kwa ajili ya watu wa Palestina, akitoa wito kwa wafuasi wake kushiriki katika kampeni hiyo. Itakumbukwa kuwa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limeonya kuhusu vifo vingi vya watoto katika Ukanda wa Gaza huku kukiwa na ukosefu mkubwa wa chakula na upatikanaji wa maji salama na huduma za matibabu katika eneo hilo. Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, UNRWA imesema kwamba "watoto katika Ukanda wa Gaza wanakufa polepole mbele ya macho ya ulimwengu." Kauli hiyo umetolewa kufuatia vifo vya watoto 15 wa Kipalestina vilivyotokana na upungufu wa maji mwilini na utapiamlo katika Hospitali ya Kamal Adwan, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Jumapili wiki iliyopita pia Umoja wa Mataifa ulionya kwamba vifo vya watoto "vitaongezeka sana" huko Gaza ikiwa misaada ya kibinadamu haitaongezeka haraka iwezekanavyo.