Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

11 Machi 2024

14:44:24
1443705

Iran: Msaada wa kimaonyesho wa US kwa Gaza ni mchezo mchungu wa kuigiza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani kile alichokitaja kuwa onyesho chungu la kipropaganda la Marekani na kueleza kuwa, hatua ya Washington ya kudai kuwapa misaada ya kibinadamu Wapalestina wa Gaza, na wakati huo huo inazuia juhudi za kimataifa za usitishaji vita katika eneo hilo lililozingirwa, ni kichekesho.

Katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari hapa Tehran hii leo, Nasser Kan’ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema "Hatua ya kimaonyesho ya Marekani ya kutuma misaada ya kibinadamu ni onyesho la kuchekesha na pia la kusikitisha." 

Hivi karibuni, Marekani ilianzisha onyesho la propaganda sambamba na kukaribia uchaguzi wa rais wa nchi hiyo, ambapo imetumia ndege zake za usafiri wa jeshi kwa ajili ya kusafirisha chakula na vifaa vingine hadi Gaza. 

Wapalestina watano wameripotiwa kuuawa na vifurushi vya misaada vilivyodondoshwa na ndege za Marekani na washirika wake kwenye Ukanda wa Gaza unaozingirwa na Israel, huku mamlaka ya Gaza ikilishutumu zoezi hilo kuwa ni "propaganda tupu" na sio huduma ya kibinadamu.

Kan'ani ameeleza kuwa, Marekani ndiyo chanzo cha kuendelea vita dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza kwa kuendelea kuipa Israel shehena za silaha. 

Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, misaada ya Iran kwa ajili ya Wapalestina wa Gaza imekwama katika badari za Misri. "Hatuwezi kutuma misaada moja kwa moja, na kwa masikitiko, Misri haijairuhusu Jamhuri ya Kiislamu kutuma misaada moja kwa moja kutokana na mazungumzo yake na Israel," ameongeza Kan'ani.Amesema shirika la Hilali Nyekundu la Iran linaendelea kuwasiliana na nchi za Kiislamu kuhusu udharura wa misaada hiyo kuwafikia Wapalestina wa Gaza haraka iwezekanavyo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema nchi za Kiislamu zinatazamiwa kuchukua hatua zaidi za kuwapa himaya Wapalestina katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kuongeza kuwa, "Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ilitarajiwa itumie ushaishi wake kuushunikiza utawala wa Kizayuni, lakini kwa bahati mbaya hatujalishuhudia hilo." Kuhusu Siku ya Kimataifa ya Quds, Kana'ani amesema anatumai mataifa yote ya dunia yatajitokeza kwa wingi kushiriki katika maandamano hayo ya Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kutangaza mshikamano na Wapalestina wanaodhulumiwa, sanjari na kulaani jinai za Wazayuni na washirika wao.