Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

11 Machi 2024

14:45:01
1443706

Kufutwa akaunti za mitandao ya kijamii za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, kielelezo cha uhasama wa Magharibi dhidi ya uhuru wa kusema

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema, hatua ya Shirika la Kimarekani la "Meta" (Facebook ya zamani) ya kufuta akaunti za mitandao ya kijamii za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kielelezo cha uhasama na uadui wa Magharibi dhidi ya uhuru wa kusema na kutoa maoni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian, ameandika makala kwenye tovuti ya habari ya Middle East Eye yenye makao yake mjini London, Uingereza, ambapo mbali na kukanusha madai ya shirika la Meta ya kufuta akaunti za mitandao ya kijamii ya Kiongozi Muadhamu katika Facebook na Instagram amesema, kauli mbiu za uhuru wa kutoa maoni zinazotolewa na baadhi ya Wamagharibi wanaojigamba kuwa watetezi wa suala hilo ni maneno matupu na wenzo tu wa kufikia malengo haramu ya kisiasa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, kufuta na kuzifunga akaunti za mitandao ya kijamii za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika intaneti si tu kunakinzana na uhuru wa kusema na kutoa maoni bali pia ni dharau kwa mamilioni ya wafuatiliaji wa misimamo na mitazamo yake kuhusu masuala muhimu ya kieneo na kimataifa. Katika hatua ya kiuadui na inayopingana na uhuru wa kutoa maoni, Shirika la Meta (Meta Platforms), ambalo hadi kabla ya mwaka 2021 lilikuwa likifanya kazi kwa jina la Facebook, lilitangaza kitambo si kirefu nyuma kuwa limechukua hatua ya kufuta akaunti za intaneti za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwenye Instagram na Facebook. Katika kuhalalisha hatua yake hiyo, Meta imedai kuwa imefanya hivyo kwa sababu akaunti za Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatullah Khamenei, zimekiuka sera za shirika hilo kuhusiana na taasisi na watu hatari. Kabla ya hapo, akaunti za mitandao ya kijamii za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ziliwekewa mipaka na hata kufutwa kwenye majukwaa mengine ya Magharibi likiwemo la Twitter. Na hii katika hali ambayo, hotuba alizotoa Ayatullah Khamenei katika miezi ya karibuni -za miito kwa Waislamu duniani kuunga mkono Muqawama wa Palestina; na wananchi wa mataifa kutoa mashinikizo kwa serikali zao katika eneo ya kuvunja uhusiano na utawala wa Kizayuni baada ya jinai za utawala huo katika ardhi za Palestina hususan Ukanda wa Ghaza-, mbali na kuungwa mkono na kupokewa kwa mtazamo chanya na watu wa eneo hili, zimewaudhi na kuwakasirisha viongozi na vyombo vya habari vya Magharibi. Kwa sababu hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani hatua isiyo ya kiungwana ya Shirika la Meta ya kufuta akaunti za mitandao ya kijamii za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ikiamini kuwa, Ayatullah Khamenei ndiye sauti inayosikika kwa wazi zaidi ya muungaji mkono wa wananchi madhulumu wa Palestina na Ghaza duniani; na kwamba vyovyote itakavyokuwa, mtandao wa vyombo vya habari vya Magharibi hautaweza kuizuia sauti hiyo isizifikie fikra za waliowengi ulimwenguni.Hasira za Wamagharibi kwa uungaji mkono wa Kiongozi Muadhamu kwa piganio tukufu la Palestina na matukio yanayojiri hivi sasa huko Ghaza, pamoja na mienendo isiyo na sababu ya majukwaa ya intaneti ya Kimarekani ya kuzifuta baadhi ya kauli za Ayatullah Khamenei na waungaji mkono wa Wapalestina wa Ghaza walioachwa bila ya makazi, zinashuhudiwa katika hali ambayo Wapalestina zaidi ya elfu 30 wameshauawa shahidi katika mashambulizi ya muda wa miezi mitano ya Wazayuni huko Ghaza, lakini hadi sasa, shirika hilo la Meta halijaweza kuonyesha msimamo wowote wa kupinga mienendo na viotendo vya kinyama na kishenzi vya Wazayuni. Akaunti za Kiongozi Muadhamu zinafungwa au kufutwa katika hali ambayo, katika miaka ya hivi karibuni, shakhsia, viongozi na hata raia wa kawaida wa nchi za Magharibi wametumia kila kisingizio katika mitandao ya kijamii kueneza chuki dhidi ya Uislamu na kukivunjia heshima Kitabu kitakatifu cha Waislamu cha Qur'ani pamoja na Mtume wao. Kuwaunga mkono wanaoivunjia heshima dini tukufu ya Uislamu yenye wafuasi wapatao bilioni mbili kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni katika nchi za Magharibi ni mfano mwingine wa mgongano na sera kiundumakuwili za nchi za Magharibi katika kutetea uhuru wa kusema na haki za binadamu. Ijapokuwa uhuru wa kutoa maoni ni miongoni mwa masuala makuu ambayo madola ya Magharibi yanayapigia upatu, lakini historia inaonyesha kuwa katika uga wa siasa, madola hayo huwa yanakubaliana na sera fulani ikiwa tu itaendana na maslahi na thamani zao. Lakini mkabala wa hilo, Uislamu unatilia mkazo kuwa na uhuru wote na wala hauwatafautishi kwa sababu ya asili, dini na rangi zao. Kwa sababu hiyo, hatua ya Shirika la Meta ( Facebook ya zamani) ya kuifuta akaunti ya Kiongozi Muadhamu si tu inaweza kuchukuliwa kuwa ni kielelezo cha wazi cha misimamo ya kiundumakuwili ya nchi za Magharibi katika suala la uhuru wa kutoa maoni, bali pia inapasa kuchukuliwa kuwa ni hatua ya kuushajiisha na kuuhamaisha utawala wa Kizayuni uendeleze jinai zake huko Ghaza. Pamoja na hayo, tajiriba ya miaka 45 ya Mapinduzi ya Kiislamu imeonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu na viongozi wake hususan Imamu Khomeini (MA) na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi Ayatullah Khamenei, hawahofishwi kamwe na vitisho, vikwazo na mashinikizo ya vyombo vya habari katika njia ya kutetea haki na uhuru wa taifa la Iran na mataifa mengine yanayodhulumiwa likiwemo la Palestina; na hatua ya kisiasa na isiyo ya kitaaluma iliyochukuliwa hivi karibuni na shirika la Kimarekani la Meta ya kuzifunga akaunti za mitandao ya kijamii za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ili kuzima sauti za upinzani na waungaji mkono wa mataifa yanayodhulumiwa duniani hususan Wapalestina wa Ghaza, itazidisha tu mwamko, uungaji mkono na uelewa zaidi wa Waislamu katika kupigania haki zao na za taifa madhulumu la Palestina.../