Main Title

source : Parstoday
Jumanne

12 Machi 2024

19:40:20
1443992

Iran, China na Russia zafanya mazoezi ya tano ya pamoja ya kijeshi katika Ghuba ya Oman

Majeshi ya wanamaji ya Iran, China na Russia leo yameanza mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika Ghuba ya Oman, yakiwa ni mazoezi ya tano ya pamoja kufanywa na majeshi hayo katika miaka ya hivi karibuni.

Manuva hayo ya pamoja ya kijeshi yanafanyika huku eneo hili likishuhudia mvutano mkubwa kutokana na vita vya vinyama vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa kwa mwezi wa sita sasa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, sambamba na hatua ya Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen ya kuzishambulia meli za utawala huo wa Kizayuni na za waitifaki wake katika Bahari Nyekundu katika kuwaunga mkono Wapalestina.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema mazoezi hayo yatakayoendelea hadi Ijumaa na kuhusisha manowari na vyombo vya anga yatajikita katika kusimamia ulinzi wa "shughuli za kiuchumi za baharini".

Vyombo vya habari vya Serikali ya Moscow vimeripoti kuwa kundi la meli za kivita za nchi hiyo kutoka Bahabri ya Pasifiki likiongozwa na Manowari ya Varyag, ziliwasili katika bandari ya Chabahar ya Iran jana Jumatatu kabla ya mazoezi ambayo yatajumuisha pia wawakilishi wa vikosi vya wanamaji wa Azerbaijan, India, Kazakhstan, Oman, Pakistan na Afrika Kusini vitakavyoshiriki kama watazamaji.

Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya China imesema mazoezi hayo - yaliyopewa jina la "Ukanda wa Usalama wa Baharini - 2024" - yanalenga "kudumisha kwa pamoja usalama wa baharini wa kikanda".

Taarifa ya wizara hiyo imebainisha kuwa "China itatuma katika mazoezi hayo  manowari ya makombora ya utunguaji ya Urumqi, manowari ya kombora ya doria ya Linyi na manowarii kubwa ya usambazaji ya Dongpinghu".

Wakati huohuo, vyombo vya habari vya Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimeripoti kuwa lengo la manuva hayo pamoja na mambo mengine, ni kuimarisha "usalama wa biashara ya kimataifa ya baharini, kupambana na uharamia na ugaidi wa baharini".

Mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Iran, China na Russia yanafanyika wakati muungano wa majeshi ya wanamaji unaoongozwa na Marekani umepiga kambi katika eneo la maji ya Bahari Nyekundu tangu Desemba 2023 kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kukabiliana na mashambulio ya Wahouthi wa Yemen dhidi ya meli za biashara zinazopita katika eneo hilo.../

342/