Main Title

source : Parstoday
Jumanne

12 Machi 2024

19:49:14
1444003

Tume ya kutafuta ukweli; wenzo wa kisiasa unaotumiwa na Magharibi dhidi ya Iran

Tume ya Umoja wa Mataifa ya kutafuta ukweli imetoa ripoti yake yenye tuhuma hewa na zisizo na msingi dhidi ya Iran, na kuonyesha kwa mara nyingine tena jinsi Wamagharibi wanaojinasibu kuwa watetezi wa haki za binadamu wanavyozitumia nyenzo za kimataifa kufikia malengo yao ya kisiasa.

Tume hiyo iitwayo eti ya kutafuta ukweli, ambayo iliundwa Desemba 2022 kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi, hususan Marekani, Uingereza na Ujerumani pamoja na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel baada ya kufeli na kugonga mwamba mradi wa kuzusha machafuko na kuvuruga amani ndani ya Iran, imetoa ripoti iliyojaa maelezo yaliyoratibiwa ya upotoshaji ukweli na uzushaji tuhuma dhidi ya Iran na kudai kwamba ukiukaji wa haki za binadamu na jinai dhidi ya ubinadamu zimefanyika hapa nchini.

Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kutafuta Ukweli, ambayo inajulikana pia kama Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa, ni tume inayoundwa kwa agizo la umoja huo au na taasisi zake tanzu kama Baraza la Haki za Kibinadamu, na kupewa jukumu la kufichua ukweli kwa mtazamo mpana, kwa wakati unaostahiki na kwa muelekeo usio na upendeleo katika maeneo yenye matatizo duniani.

Hii ni pamoja na ukweli kwamba, uzoefu na tajiriba ya miongo ya hivi karibuni inaonyesha wazi kwamba, nchi za Magharibi kwa upande mmoja zinajaribu kuzitafsiri haki za binadamu kwa kutumia vigezo vyao; na kwa upande mwingine, zinatumia nyenzo za kimataifa kama Tume za Kutafuta Ukweli na Baraza la Haki za Binadamu kufanikisha malengo yao ya kisiasa na vilevile kuziwekea mashinikizo nchi zenye misimamo huru.

Hoja muhimu zaidi ya kuthibitisha dai hili ni kushuhudia kuundwa kwa Tume za Kutafuta Ukweli za kuzichunguza baadhi ya nchi tu na kuzipa kinga ya kutozifuatilia nchi za Magharibi zinazojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu pamoja na washirika wao; hali ya kuwa kuna ushahidi chungu nzima unaothibitisha ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa katika nchi za Magharibi.

Kuhusiana na suala hilo, kufuatia machafuko yaliyozuka Septemba 2022 katika baadhi ya miji ya Iran, nchi za Magharibi zilipaza sauti zao kwa mara nyingine tena kunadi kuwa zinatetea haki za binadamu za wananchi wa Iran, ilhali maisha ya mamilioni ya wananchi hao yanaatilika vibaya sana kutokana na vikwazo haramu ilivyowekewa Iran na nchi hizo.

Ghasia na machafuko ya 2022 yalitoa fursa pia kwa Wamagharibi wanaojinasibu kuwa watetezi wa haki za binadamu kuendeleza uadui wao wa kisiasa wa muda mrefu dhidi ya Iran kupitia vyombo vya haki za binadamu. Kwa kutegemea ripoti na taarifa zilizotolewa na watu binafsi, vyombo vya habari na makundi yenye uhasama na uadui na Jamhuri ya Kiislamu, Wamagharibi hao walianza kutengeza habari na takwimu za kubuni dhidi ya Iran, na kwa njia hiyo wakachukua hatua ya hata kufuta uanachama wa Iran katika Kamisheni ya Kimataifa ya Hadhi ya Mwanamke.

Ni kwa sababu hiyo, ndio maana tangu ilipotangazwa kuundwa tume hiyo eti ya kutafuta ukweli, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisisitiza na kutamka bayana kuwa haitaitambua tume hiyo na itazichukulia ripoti zake itakazotoa kuwa ni kitu kisicho na itibari wala uhalali wowote wa kisheria. Na huo ndio msimamo ambao Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliutilia mkazo kwa mara nyingine tena siku ya Jumamosi baada ya kutolewa ripoti rasmi ya tume hiyo.