Main Title

source : Parstoday
Jumatano

13 Machi 2024

20:40:16
1444244

HAMAS yakanusha madai ya kukubali pendekezo la usitishaji vita

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekadhibisha ripoti ya shirika la habari la al-Arabiya kwamba kundi hilo la muqawama limeafiki 'pendekezo la kimataifa' la usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa, HAMAS imepuuzilia mbali ripoti hiyo ya al-Arabiya ikisisitiza kuwa, chombo hicho cha habari kinapasa kuhakikisha kuwa habari kinazochapisha ni za uhakika, ukweli na za kuaminika.

Harakati hiyo ya muqawama ya Palestina imebainisha kuwa, vyombo vya habari vina wajibu wa kujiepusha na tabia ya kucheza na hisia za watu hasa Wapalestina, wakati huu ambao jeshi la utawala wa Kizayuni linaendelea kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

HAMAS imesisitiza kuwa, ripoti ya shirika la habari la al-Arabiya kwamba ujumbe wa HAMAS ndani ya siku chache zijazo utaelekea Cairo, Misri kujadili na kusaini makubaliano ya kuanza kutekeleza kile kilichotajwa kuwa pendekezo la kimataifa la usitishaji vita, haina itibari.Kabla ya hapo, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS alisema hakutakuwa na makubaliano yoyote na utawala haramu wa Israel kabla ya utawala huo pandikizi kusimamisha kikamilifu hujuma zake dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuyaondoa majeshi yake katika eneo hilo. "Hatutaki makubaliano ambayo hayatamaliza vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza au kuhakikisha watu wetu waliofukuzwa makwao wanarejea katika makazi yao, au makubaliano ambayo hayatoi hakikisho la kuondoka kwa adui Mzayuni katika Ukanda wa Gaza", alisema Ismail Haniyah. HAMAS inasisitiza kuwa, makubaliano yoyote ya usitishaji vita Gaza lazima yajumuishe dhamana ya kimataifa ili kuulazimisha utawala ghasibu wa Israel kuyatekeleza.