Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

15 Machi 2024

13:55:44
1444568

Mashambulio pacha ya jeshi la Kizayuni yaua Wapalestina 29 waliokuwa wakingojea msaada wa chakula Ghaza

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limewaua shahidi Wapalestina wapatao 29 wakati wakisubiri msaada katika mashambulizi mawili tofauti lililofanywa dhidi ya Ukanda wa Ghaza uliozingirwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina huko Ghaza, katika tukio la kwanza la hapo jana Alkhamisi, Wapalestina wanane waliuawa shahidi katika shambulio la anga kwenye kituo cha usambazaji misaada katika kambi ya Al Nuseirat katikati mwa Ghaza. Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kwamba, baadaye, Wapalestina wengine 21 waliuawa na zaidi ya 155 walijeruhiwa kwa risasi baada ya askari wa jeshi la Kizayuni kushambulia umati wa watu waliokuwa wakisubiri malori ya misaada katika mzunguko wa kaskazini wa Ghaza. Katika upande mwingine, madaktari wa Palestina wameripoti kuwa, kombora la jeshi la utawala wa Kizayuni lilipiga nyumba jana Alhamisi huko Deir al Balah katikati mwa Ghaza na kuua shahidi watu tisa.Na katika kile kinachoonekana kama desturi yake hivi sasa, jeshi la Israel limekanusha kushambulia vituo vya misaada. Wapalestina wa Ghaza wamesema, mashambulizi ya anga na ardhini ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni yaliendelea usiku kucha katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Rafah kusini, ambako zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao wametafuta hifadhi. Mashambulizi ya kigaidi ya jeshi la Israel yamewafanya akthari ya Wapalestina zaidi ya milioni 2.3 walazimike kuyahama makazi yao. Mnamo Februari 29, wanajeshi wa Israel waliwaua kwa risasi zaidi ya Wapalestina 100 walipokuwa wakisubiri kupatiwa msaada karibu na Mji wa Ghaza. Na kama kawaida yake, utawala wa Kizayuni ulijivua na dhima ya mauaji hayo na kuwalaumu Wapalestina waliouawa kwamba walijisababishia wenyewe vifo vyao.../