Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

15 Machi 2024

13:56:35
1444570

Abbas amkabidhi Mohammed Mustafa jukumu la kuunda Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina

Rais Mahmoud Abbas wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amemteua Mohammed Mustafa kuwa Waziri Mkuu mpya na kumkabidhi jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri la serikali hiyo.

Kwa mujibu wa IRNA, duru za Palestina zimeripoti kuwa: Abbas amemteua Mustafa na kumkabidhi jukumu hilo la kuunda serikali licha ya kuwepo upinzani ndani ya harakati ya Fat-h. Duru hizo za Palestina zimeeleza pia kwamba, Muhammad Mustafa ndilo chaguo lililokubaliwa na Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu. Katika taarifa yake ya kutangaza uteuzi huo  jana Alkhamisi, Abbas alimtaka Mustafa kuweka pamoja mipango ya kuunganisha tena utawala katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Ukanda wa Ghaza uliowekewa mzingiro, kuongoza mageuzi katika serikali, vyombo vya usalama na uchumi na kupambana na rushwa.

Mustafa anachukua nafasi ya Waziri Mkuu wa zamani Mohammed Shtayyeh ambaye, pamoja na serikali yake, walijiuzulu mwezi Februari akielezea haja ya mabadiliko wakati huu wa vita vya kinyama vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza na kuongezeka kwa hujuma na mashambulio ya jeshi la Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina inayotambuliwa na Jamii ya Kitaifa na inayoongozwa na harakati ya Fat-h, ina mamlaka yenye mipaka maalumu ya kujiendeshea mambo yake katika Ukingo wa Magharibi, lakini ilipoteza udhibiti wa Ghaza kwa Hamas mwaka 2007 baada ya harakati hiyo ya Muqawama kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Bunge la Palestina.

Wawakilishi wa harakati za Fat-h na Hamas wanatarajiwa kukutana mjini Moscow, Russia wiki hii kwa mazungumzo.../

342/