Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

15 Machi 2024

13:57:12
1444571

'Wapalestina ndio wataamua mustakbali wao baada ya vita vya Ghaza, si wavamizi'

Kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, wananchi wa Palestina ndio watakaoamua mustakbali wao baada ya vita vya Ghaza na hawatopangiwa mambo yao na Wazayuni wavamizi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Osama Hamdan amesema hayo baada ya kikao baina ya ujumbe wa ngazi za juu wa HAMAS na Katibu Mkuu wa Hizbulla ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah.

Osama Hamdan ameongeza kuwa kikao chao hicho na Sayyid Hassan Nasrallah ni sehemu ya mfululizo wa vikao vya mara kwa mara kati ya Hizbullah na viongozi wa Hamas na wamejadiliana mambo matatu ya kimsingi.

Kiongozi huyo wa HAMAS amesema hayo kwenye mahojiano na televisheni ya Al-Jadeed na kuongeza kuwa, kikao chao hicho kimejadili matukio ya Ghaza, msimamo wa kisiasa kuhusu matukio ya kieneo kutokana na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni pamoja na juhudi za kisiasa zinazofanywa na duru mbalimbali za kukomesha jinai hizo yakiwemo mazungumzo ya hivi karibuni ya Cairo, Misri.Vilevile amejibu madai yaliyotolewa na maafisa wa Israel kuhuhu Ghaza na kusema kuwa, Wapalestina wenyewe ndio watakaoamua mustakbali wao, si wavamizi. Matamshi hayo ya Hamdan yamekuja baada ya vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni kudai kuwa Israel ina nia ya kukabidhi uendeshaji wa Ukanda wa Ghaza mikononi mwa Majid Faraj, Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Vyombo hivyo vimedai pia kuwa, Faraj eti ataunda kikosi cha kijeshi ambacho kitasimamia usalama wa Ukanda wa Ghaza, madai ya kichochezi ambayo yamepingwa vikali na makundi ya muqawama ya Palestina.


/342