Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

15 Machi 2024

13:57:52
1444572

Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran: Hali ya Gaza inamfanya kila mwanadamu alie machozi ya damu

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amelitaja suala la Gaza na Palestina kuwa ndiyo kadhia ya kwanza ya Ulimwengu wa Kiislamu.

Katika hotuba za Swala ya Ijumaa ya Tehran, Hujjatul-Islam Walmuslimin Kazem Seddiqi ameashiria jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Gaza na kuzikosoa baadhi ya nchi za Kiarabu akisema: Inatarajiwa kuwa serikali za nchi hizo zitavunja uhusiano wao na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwatetea watu wa Palestina na Gaza.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameeleza kuwa, licha ya matatizo makubwa ya raia, vita vya Gaza vinadhihirisha baadhi ya hakika ikiwa ni pamoja ni jinai na uhalifu usio na kikomo wa Marekani na kibaraka wake Israel, ambayo haina mipaka katika kutenda uhalifu. Amesema Marekani na Israel zimeua watu wasio na ulinzi, kushambulia wagonjwa hospitalini na kuwaangamiza watoto katika eneo la Gaza lisilo na chakula, maji, dawa, usalama wala makazi.

Hujjatul-Islam Walmuslimin Kazem Seddiqi amesisitiza kuwa, hali hii inamfanya kila mwanadamu alie machozi ya damu.Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amehoji kwamba: Kwani watu wa Gaza sio wanadamu na Waislamu? Kwa nini nchi za Kiarabu zinazojiita Waislamu hazikati uhusiano wao na Israel, na baadhi ya nchi hizo zinausaidia utawala huo dhidi ya wanamapambano wa Palestina?

Katika sehemu nyingine ya hotuba za Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran, Hujjatul-Islam Kazem Seddiqi amezungumzia baraka za mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusema: “Katika mwezi huu mtukufu, nyoyo za waumini wote duniani zinakuwa na rangi moja, kila mtu anajiweka mbali na dhambi na maasi na Waislamu wanashiriki katika Swala za jamaa misikitini kwa shauku kubwa." Amesisitiza kuwa, miongoni mwa baraka kubwa zaidi za mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kujenga umoja na mshikamano baina ya Waislamu.Amewahimiza Waislamu kuzidisha taqwa na uchamungu katika mwezi huu na kushikamana na Qur'ani ambayo iliteremshwa katika mwezi wa Ramadhani na kusema: Viwili hivyo, yaani mwezi Ramadhani na Qur'ani, vitatoa shafaa na maombezi Siku ya Kiyama.  

342/