Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

15 Machi 2024

14:00:14
1444577

Kurefushwa hali ya hatari kitaifa; muendelezo wa mtazamo wa uadui wa Marekani dhidi ya Iran

Siku ya Jumanne, Rais Joe Biden wa Marekani alirefusha kwa mwaka mwingine mmoja, muda wa hali ya hatari ya kitaifa kuhusu Iran. Tangu 1995, marais wote wa Marekani wamekuwa wakirefusha kila mwaka hali hiyo iliyoanza kutekelezwa kupitia Agizo la Utendaji nambari 12957 dhidi ya Iran.

Mnamo Machi 15, 1995, Rais Bill Clinton wa Marekani, alitangaza hali ya hatari ya kitaifa dhidi ya Iran kwa madai ya kukabiliana na eti vitisho visivyo vya kawaida vinavyotokana na sera za serikali ya Iran dhidi ya maslahi ya kitaifa, sera za kigeni na uchumi wa Marekani.

Kabla ya hapo, Rais Jimmy Carter wa nchi hiyo, alikuwa tayari ametoa Agizo la Utendaji nambari 12170 mnamo Novemba 14, 1979, yaani, siku 10 baada ya kutekwa pango la ujasusi la Marekani mjini Tehran, lililoamrisha kufungiwa mali zote za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Marekani, na kuanzia mwaka huo hadi sasa marais wote wa Marekani wamekuwa wakirefusha agizo hilo.

Kitendo cha Biden kurefusha hali ya hatari dhidi ya Iran kinaonyesha mwelekeo halisi wa Marekani kuhusu Iran, ambao ni mwendelezo wa uadui na uhasama dhidi ya taifa la Iran. Tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, Marekani, ikijiona kuwa kinara wa kambi ya Magharibi ambayo imekuwa ikijaribu kila mara kutekeleza nafasi ya kibabe katika eneo la Asia Magharibi, imezipa kipaumbele siasa za chuki na uadui dhidi ya Iran na kutekeleza njama nyingi za kujaribu kuipindua serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Marekani imekuwa ikitekeleza sera na hatua za upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama vile kuiwekea vikwazo vikali ambavyo vimetajwa kuwa ni vya kulemaza, vitisho vya kijeshi, kuanzisha kampeni za kisiasa na kidiplomasia na vita vya kisaikolojia dhidi ya Tehran.Licha ya kutokuwa na tija siasa hizo za uhasama, lakini Washington bado inasisitiza juu ya kuendeleza mbinu hiyo dhidi ya Tehran ambayo ni kinyume cha Hati ya Umoja wa Mataifa, ambapo katika kipindi hiki cha utawala wa Joe Biden, alianzisha na kushadidisha vita mseto dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa visingizio tofauti visivyo na msingi. Tangu aingie madarakani Januari 2021, na kinyume na kauli mbiu zake za awali, Biden ameendeleza kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa ambapo mara kwa mara hutangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran.

Mwenendo wa Iran kuwekewa vikwazo vikali na visivyo vya kawaida ulipata sura na muelekeo mpya katika kipindi cha utawala wa Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani, baada ya nchi hiyo ya Magharibi kujitoa katika mkataba wa nyuklia wa JCPOA na kisha kuanzisha kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran. Marekani imekuwa ikitekeleza vikwazo vikali dhidi ya Iran kwa matarajio kuwa inaweza kuilazimisha isalimu amri mbele ya vitendo na matakwa yake yasiyo ya kimantiki na haramu, jambo ambao bila shaka limeshindwa kutimia kama zinavyokiri serikali tofauti za Marekani yenyewe, ikiwemo hii ya Biden. Aidha marais wa Marekani, hususan George W. Bush, kwa kuijumuisha Iran katika kile kinachoitwa mhimili wa shari, mara kadhaa walitishia kuishambulia kijeshi Iran, lakini bila shaka vitisho hivyo havikutekelezwa kutokana na nguvu kubwa ya Iran. Wakati wa utawala wa Barack Obama, sera za kuiwekea vikwazo na kuitishia Iran ziliendelea, ambapo utawala wake ulikuwa ukidai mara kwa mara kwamba machaguo yote kuhusu Iran yalikuwa yako mezani, ukimaanisha uwezekano wa Iran kushambuliwa kijeshi. Hata hivyo, jibu kali la Iran kwa tishio lolote la Marekani limemfanya hata rais wa zamani wa Marekani na mwenye utata mwingi, Donald Trump, asithubutu kutekeleza tishio lake la eti kutaka kushambulia nukta 52 katika ardhi ya Iran.

Kwa kuzingatia kwamba Merekani inajiandaa kufanya uchaguzi wa rais mwaka huu, Donald Trump, akiwa mgombea wa chama cha Republican katika kampeni zake za uchaguzi, anajaribu kuvutia upande wake kura za lobi za Wazayuni nchini humo, ikiwemo ya AIPAC. Bila shaka Joe Biden, akiwa mgombea wa chama cha Democrats katika uchaguzi huo, pamoja na maafisa wakuu wa serikali yake, wanajaribu kuzidisha vikwazo vilivyopo na kutumia vitisho na maneno makali dhidi ya Iran ili nao wapate fursa ya kuzoa kura hizo.