Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

16 Machi 2024

19:33:54
1444904

UNRWA: Itachukua miaka kuondoa tani milioni 23 za vifusi Gaza

Vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni wa Israeli dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza hadi sasa vimeacha takribani tani milioni 23 za vifusi na silaha ambazo hazikulipuka katika eneo hilo. Hayo yamedokezwa Ijumaa na wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa.

Katika tahadhari mpya kuhusu hali mbaya ya dharura ya kibinadamu ambayo bado inatokea katika eneo hilo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limesema kwamba "itachukua miaka" kabla ya Ukanda huo kuwekwa salama na kurejea tena katika hali ya kawaida.

Maisha ya zaidi ya watu milioni mbili wa Gaza yameharibiwa na mashambulizi ya kila siku ya utawala haramu wa Israel, tangu tarehe 7 Oktoba, UNRWA imeeleza katika chapisho kwenye mtandao wa X, zamani Twitter.

UNWRA ikiwa ndilo shirika kubwa zaidi la misaada huko Gaza linaendelea kutoa vifaa na huduma za kuokoa maisha kwa zaidi ya watu milioni 1.5 waliokimbia makazi yao kusini mwa eneo hilo. Shirika hilo linaendesha makazi kwa zaidi ya watu milioni moja, kuwapa misaada ya kibinadamu na huduma ya afya ya msingi.

Kazi ya kuokoa maisha ya kibinadamu inaendelea huku kukiwa na mashambulizi makali ya Israel ya mabomu na operesheni za ardhini pamoja na mapigano makali kati ya majeshi ya Israel na makundi yenye silaha ya Palestina.

Katika taarifa yake ya hivi punde kuhusu hali ya dharura, ofisi ya uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa, OCHA, inaripoti kwamba ghasia zingali zinaendelea "katika sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza, hasa katika eneo la Hamad la Khan Younis. Mapigano hayo yanasababisha vifo zaidi vya raia, kufurushwa na uharibifu wa nyumba na miundombinu mingine ya raia.”

Israel ilianzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari Gaza mnamo Oktoba 7, 2023. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, wapalestina wasiopungua 31,000 wameuawa na zaidi ya 73,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel. Takriban asilimia 72 ya waathiriwa ni watoto na wanawake.

Zaidi ya miezi mitano ya mashambulizi ya kikatili ya Israel pia yamesababisha njaa kali miongoni mwa Wagaza huku takribani asilimia 60 ya miundomsingi ya eneo hilo ikiwa imeharibiwa.