Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

16 Machi 2024

19:36:29
1444907

Iran yatiwa wasiwasi na kushtadi kampeni za chuki dhidi ya Uislamu

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu inatiwa wasiwasi na hatua ya kupanuka mtandao wa kampeni za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu duniani.

Amir Saeid Iravani alisema hayo jana Ijumaa katika mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu.

Ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inalaani vikali vitendo na kauli za chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu, na vile vile mashambulizi ya kigaidi na wimbi la uhalifu dhidi ya Waislamu, na dhidi ya imani, mafundisho na matukufu ya Kiislamu.

Iravani ameeleza kuwa: Huku ikielezea hofu yake kuhusiana na kutanuka kwa kiwango kikubwa mtandao wa kampeni za chuki dhidi ya Uislamu, Jamhuri ya Kiislamu inalaani vikali kauli yoyote ya chuki na ubaguzi, mashambulizi ya kigaidi na hujuma dhidi ya Waislamu na matukufu yao.Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, makundi ya watu wanaounga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel yameanzisha kampeni kubwa dhidi ya Uislamu kote duniani, na kwamba makundi hayo yanaeneza chuki sio tu dhidi ya Palestina, bali pia dhidi ya nchi nyingine za Kiislamu. Uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu umeongezeka katika nchi mbalimbali duniani, baada ya kuanza kwa mashambulizi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza Oktoba 7, 2023. Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa, Uislamu haungi mkono ugaidi na misimamo ya kufurutu ada, na kwamba vitendo vya kigaidi havipasi kuoanishwa na dini, taifa, ustaarabu na kundi lolote la kijamii.

342/