Main Title

source : Parstoday
Jumapili

17 Machi 2024

20:11:59
1445190

Hamdan: Mpango uliopendekezwa na HAMAS kwa ajili ya kusitisha vita unaendana na uhalisia

Osama Hamdan, mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, mpango uliopendekezwa hivi karibuni na harakati hiyo kwa ajili ya usitishaji vita unaendana kikamilifu na uhalisia wa mambo kwa namna ambayo adui hawezi kuukataa.

Kwa mujibu wa IRNA, Hamdan ameeleza kwamba wakati wa mazungumzo, Hamas imetaka kusitishwa vita, kurejea wakimbizi, kutolewa misaada na kuanza ujenzi mpya wa Ghaza, na akasema: "katika mpango huu, tuliwasilisha maelezo ya kina kuhusiana na suala la mateka na kuondoka vikosi vya utawala ghasibu katika eneo la Ghaza". Kiongozi huyo wa Hamas amebainisha kuwa harakati hiyo inasubiri majibu ya utawala wa Kizayuni na Marekani ikiwa ni muungaji mkono wa utawala huo katika vita dhidi ya Ghaza na akasema: "Tunashuhudia tofauti na migongano ndani ya baraza la mawaziri la utawala huo ghasibu'. Huku akisisitiza kuwa utawala wa Kizayuni haujafikia hata moja kati ya malengo uliyokusudia katika vita vya Ghaza, kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesema: "Benjamin Netanyahu anajua ni vipigo gani ambavyo jeshi la utawala huo limepata huko Ghaza".

Wakati huohuo, Ahmed Abdul Hadi, mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon amesema katika mahojiano na mtandao wa Al-Mayadeen Jumamosi usiku: "Makubaliano ya kubadilishana mateka yanawezekana tu kwa kusitishwa kikamilifu uvamizi wa kijeshi dhidi ya Ghaza."

 Abdul Hadi ameongeza kuwa: siku mbili zilizopita, Hamas iliwasilisha maoni yake, ambayo yanajumuisha masharti yanayozingatia hatua tatu kwa ajili ya kusimamisha mashambulio dhidi ya Ghaza na kuanza mazungumzo. Ameongeza kuwa: katika suala la mateka Hamas imeonyesha ulainifu, lakini suala hilo litawezekana tu kwa kusitishwa kikamilifu uchokozi na kutolewa dhamana na mahakikisho ya kimataifa. Mwakilishi huyo wa Hamas nchini Lebanon ameongeza kuwa: mpira huo sasa uko kwenyea uwanja wa (utawala wa) Israel na Marekani, lakini inaonekana kuendelea na kupanuka kwa vita ni kwa faida ya Netanyahu; kwa sababu kumalizika kwa vita kunamaanisha yeye kupandishwa kizimani na kuhukumiwa kifungo. Abdul Hadi ameendelea kusema: serikali ya Marekani inatumia vipimo vya undumakuwili na, mkabala na kauli zake kuhusu ufikishaji misaada Ghaza, haiwawekei wavamizi mashinikizo yoyote ya kuacha uchokozi wao. Mwakilishi huyo wa Hamas ameongezea kwa kusema: "leo, Muqawama una uwezo na uko imara, na unasimamia kwa ustadi mapigano katika maeneo yote ya Ukanda wa Ghaza na ungali unaendelea kuwatia hasara maadui".../


342/