Main Title

source : Parstoday
Jumapili

17 Machi 2024

20:12:45
1445193

Qatar yataka uchunguzi huru ufanyike kuhusu mauaji ya waandishi wa habari huko Gaza

Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema kuwa, Gaza imeshuhudia mauaji makubwa zaidi ya waandishi wa habari katika historia ya sasa ya vita.

Serikali ya Qatar Imesisitiza wajibu wa nchi zote kuwalinda waandishi wa habari na kuwahakikishia mazingira salama ya kufanya kazi zao kwa uhuru, na imetoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na usio na upendeleo, kwa mujibu wa viwango vya kimataifa, na kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika na mauaji ya waandishi wa habari Ukanda wa Gaza hawakwepi adhabu.

Hayo yameelezwa na Qatar mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha 55, kupitia hotuba iliyotolewa na Abdullah Nasser Al Naama, Katibu wa Tatu wa Idara ya Haki za Binadamu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, wakati wa majadiliano yaliyojikita katika "kuwalinda waandishi wa habari."

Al-Naama amesema, “Suala la kulinda na kuimarisha haki za waandishi wa habari na ongezeko la ukiukwaji wa sheria unaofanywa dhidi yao, pamoja na kukithiri hali za kukwepa adhabu na kutowajibishwa wahusika wa uhalifu huo, ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo suluhisho lake linapaswa kupatikana haraka iwezekanavyo.”

Qatar imeongeza kuwa, idadi ya waandishi wa habari waliouawa shahidi na Israel huko Gaza, tangu Oktoba 7, imefikia zaidi ya waandishi wa habari 130, wengine 16 wamejeruhiwa, 4 hawajulikani waliko, na 25 wamekamatwa na Israel. 

Afisa huyo wa Qatar amesema idadi hiyo huenda ikaongezeka na kuwa kubwa zaidi ya waandishi wa habari waliouawa katika historia ya sasa ya vita.

Abdullah Nasser Al Naama ametaka kufanyike uchunguzi wa haraka, huru na usio na upendeleo kwa mujibu wa viwango vya kimataifa, na kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika na mauaji ya waandishi wa habari huko Gaza hawakwepi kuadhibiwa. 

342/