Katika mkutano aliofanya na mwenzake wa Syria Ali Mahmoud Abbas mjini Tehran jana Jumamosi, Ashtiani alionya dhidi ya njama za Marekani na Israel za kuzidisha mgogoro katika eneo la Asia Magharibi. Amesema, kosa lolote la kistratijia na chokochoko za Marekani na utawala wa Kizayuni zitapelekea hali kuwa mbaya zaidi katika eneo hili. Brigedia Jenerali Ashtiani amelaani mashambulizi ya anga yanayofanywa na Israel dhidi ya Syria na ukiukaji wa mamlaka ya ardhi ya nchi hiyo na akasema, utawala huo ghasibu unalenga kuharibu miundombinu ya nchi hiyo kama vile viwanja vya ndege na bandari na kushambulia misafara ya kubeba mafuta na chakula kwa kisingizio cha mapambano dhidi ya Muqawama. Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema ana imani kuwa mashambulizi ya Israel yanatokana na hofu na kushindwa utawala huo ghasibu.Amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uwezo wa kuzuia hujuma ili kukabiliana na mashambulizi ya Israel na kubainisha kuwa, hatua na mipango ya lazima na ya dharura iko katika ajenda zitakazofanyiwa kazi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kukabiliana na uchokozi wa utawala huo ghasibu.
Abbas ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unaoua watoto umezidisha hali ya wasiwasi katika eneo hususan katika nchi za Syria na Lebanon baada ya kushindwa kufikia malengo yake huko Ghaza na kutumia uungaji mkono wa Muqawama na Iran kwa wananchi madhulumu wa Palestina kama kisingizio cha kuziandama nchi hizo.
Waziri wa Ulinzi wa Syria amebainisha kuwa, kuwepo kinyume cha sheria Marekani nchini Syria kumeifanya nchi hiyo kuwa kituo cha uungaji mkono kwa makundi yanayotaka kujitenga na ya kigaidi.
Aidha amekumbusha kuwa, Muqawama na kuimarishwa ushirikiano wa kiulinzi kati ya Tehran na Damascus ndio njia bora za kukabiliana na maadui.../