Main Title

source : Parstoday
Jumanne

19 Machi 2024

14:32:01
1445547

Borrell: Gaza limegeuka kaburi kubwa zaidi la wazi duniani

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya huku akieleza wasiwasi mkubwa alionao kuhusu mgogoro wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza amesema kuwa, eneo hilo la Wapalestina lililozingirwa limegeuka na kuwa kaburi kubwa zaidi la wazi duniani.

Josep Borrell alisema hayo jana Jumatatu mjini Brussels akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kukutana na mawaziri wa EU na kuongeza kuwa, "Gaza ni kaburi kubwa la makumi ya maelfu ya watu, na pia kaburi kubwa la misingi ya sheria za kibinadamu."

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya ameashiria mgogoro wa binadamu unaoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, utawala wa Israel unatumia njaa kama silaha katika vita.

Ameeleza bayana kuwa, Wapalestina wa Gaza wanaaga dunia kutokana na hatua ya Israel ya kuzuia misaada ya kibinadamu kuingine katika eneo hilo na kuongeza kuwa, mamia ya watu wanaendelea kufa kwa njaa, aghalabu yao wakiaga dunia kutokana na utapiamlo.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa EU amebainisha kuwa: Kabla ya vita, Gaza lilikuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani, lakini baada ya kuanza vita (Oktoba 7,2023), limegeuka na kuwa kaburi kubwa zaidi la wazi duniani.

Hadi sasa utawala wa katili wa Israel umewaua shahidi Wapalestina karibu 32,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto, mbali na kuwajeruhi wengine 73,676.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), zaidi ya watoto Wapalestina 13,000 wameuawa katika vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza. 

342/