Main Title

source : Parstoday
Jumanne

19 Machi 2024

14:33:45
1445550

Jeshi la Israel lashambulia tena Hospitali ya Al-Shifa, laua na kujeruhi kadhaa

Vikosi vya jeshi la utawala wa Israel vilivyojizatiti kwa silaha nzito vimevamia hospitali ya al-Shifa katika mji wa Ghaza kwa kutumia vifaru na ndege zisizo na rubani na kuwafyatulia risasi watu waliokuwa ndani ya jengo hilo.

Ofisi ya vyombo vya habari vya serikali huko Ghaza imesema uvamizi huo ambao ulifanyika mapema leo Jumatatu, umezua hofu na taharuki na kutishia maisha ya maelfu ya wagonjwa, wafanyakazi wa kada ya tiba na raia waliopoteza makazi yao waliopewa hifadhi ndani ya hospitali hiyo.


Taarifa ya ofisi hiyo imeleza kwamba, uhalifu huo mpya wa kivita umeongeza rekodi nyingine chafu katika faili la jeshi vamizi linalokalia ardhi kwa mabavu, ambalo lingali linafanya uhalifu na mauaji mengi, na linaendelea kuiangamiza sekta ya afya na kuharibu hospitali katika Ukanda wa Ghaza uliwekewa mzingiro".

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza, watu wapatao 30,000, wakiwemo raia waliopoteza makazi yao, wagonjwa waliojeruhiwa na wafanyakazi wa kada ya tiba wamekwama ndani ya hospitali hiyo ya Al-Shifa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kila anayejaribu kutoka hospitalini humo analengwa na risasi za wadunguaji na ndege zisizo na rubani.

Wakati huohuo, Harakti ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa taarifa ikisema, uhalifu wa Israel katika vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza "hautatoa taswira yoyote ya ushindi kwa Netanyahu na jeshi lake la Nazi."

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, ukatili wa Israel unaonyesha "hali ya kuchanganyikiwa, fujo, na kupoteza matumaini" ndani ya jeshi la utawala huo, ambalo halijapata mafanikio yoyote katika mashambulizi dhidi ya Ghaza.

Hamas imesema: "kushindwa Jamii ya Kimataifa na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua dhidi ya jeshi linalokalia ardhi kwa mabavu la Kizayuni kumebariki kuendelezwa vita vya mauaji ya kimbari na uangamizaji wa kizazi unaofanywa dhidi ya watu wetu".

Halikadhalika, harakati hiyo ya Mujahidina wa Palestina imesema, inaubebesha dhima -utawala wa Marekani, serikali za Magharibi, tawala za Kiarabu zilizozembea, na mfumo wa kimataifa usio na uwezo- ya kuendelea mauaji ya kimbari yanayofanywa na adui wa Kinazi na Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza, ya karibuni zaidi yakiwa ni ya kushambuliwa Hospitali ya al-Shifa katika eneo hilo.../

342/