Main Title

source : Parstoday
Jumanne

19 Machi 2024

14:34:52
1445552

Iran: Shutuma za USA na UK kuhusu Bahari Nyekundu na Yemen hazina msingi wowote

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekanusha tuhuma zisizo na msingi za Marekani na Uingereza dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu hali ya Bahari Nyekundu na Yemen.

Amir Saeid Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, jana Jumatatu alimwandika barua Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akijibu masuala yaliyowasilishwa katika kikao cha hivi karibuni cha baraza hilo kuhusu Yemen. Amesema: Katika mkutano huu, wawakilishi wa Marekani na Uingereza kwa mara nyingine tena wametumia vibaya jukwaa la Baraza la Usalama, na kutoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kuhusiana na hali ya Bahari Nyekundu na Yemen.

Iravani amefafanua kuwa: Sambamba na Tehran kukanusha kikamilifu tuhuma hizi zisizo na msingi, inazitambua kama kisingizio ambacho Washington na London zinatumia kuendeleza ajenda zao za kisiasa zenye muono fupi, na vilevile kuhalalisha na kutetea vitendo vyao haramu na uchokozi wa kijeshi dhidi ya Yemen.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga madai yasiyo na ushahidi dhidi ya Tehran katika taarifa iliyosomwa na mwakilishi wa Ufaransa katika mkutano wa Baraza la Usalama.Ameongeza kuwa: Tehran inaiomba Paris, ikiwa mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, kuchukua hatua kwa uwajibikaji zaidi, na kujiepusha kutoa tuhuma za kisiasa dhidi ya nchi nyingine huru bila ya kuwa na ushahidi. Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikiunga mkono utatuzi wa amani wa mgogoro wa Yemen kupitia njia za kidiplomasia na inatilia mkazo wajibu wake wa kulinda usalama wa baharini na uhuru wa usafiri wa baharini.

342/