Main Title

source : Parstoday
Jumanne

19 Machi 2024

14:35:25
1445553

Kuwekwa vikwazo vipya dhidi ya Iran

Wizara ya Fedha ya Marekani kwa mara nyingine imeamua kuweka vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ikitangaza habari hiyo kupitia taarifa, Wizara ya Fedha ya Marekani imesema imeuwekea vikwazo mtandao wa makampuni na watu binafsi ambao wanatuhumiwa kuhusika katika kuwezesha uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa makumi ya makampuni ya Kimarekani hadi taasisi za Iran, ikiwa ni pamoja na Benki Kuu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matawi na makampuni tanzu ya Kampuni ya Iran Informatics nchini Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE pamoja na watu watatu wanaohusiana nayo wamewekewa vikwazo, akiwemo Pouria Mirdamadi, aliye na uraia wa nchi mbili za Iran na Ufaransa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vya mara kwa mara vya Marekani kwa zaidi ya miongo minne iliyopita. Moja ya malengo muhimu ya Marekani ni kujaribu kuipigisha magoti Iran, kwa sababu, ikiwa nchi huru, imekataa kusalimu amri mbele ya matakwa haramu ya Washington, na hadi sasa mashinikizo makubwa ya nchi hiyo ya kibeberu yameshindwa kuzaa matunda wala kuvuruga harakati za Iran za kuendelea kutekeleza sera huru kitaifa na kimataifa.

Mohsen Rui Sefat, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuhusu hilo: "Tunaweza kusema bila kusita kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi pekee duniani iliyo na siasa huru zinazopingana na Marekani. Kwa hakika Iran inazidi kubadilika na kuwa nchi yenye nguvu kubwa kikanda, jambo ambalo linaitia Marekani wasiwasi mkubwa. Hii ni kwa sababu ni Iran pekee ndiyo inatoa changamoto kubwa kwa Marekani."Kwa hiyo, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza chini ya mwezi mmoja uliopita kwamba imelenga na kuwafuatilia kwa karibu watu watatu na taasisi nne zinazodaiwa kuhamisha teknolojia ya kisasa ya Marekani kwa ajili ya kutumiwa na Benki Kuu ya Iran. Hii ni katika hali ambayo Marekani kivitendo inatekeleza ugaidi wa kiuchumi dhidi ya Iran kwa kuiwekea na kuizidishia vikwazo haramu vya kiuchumi. Hata kama ugaidi kwa kawaida hutathminiwa kwa mitazamo ya kijeshi na kiusalama, lakini ni wazi kuwa Marekani inatekeleza ugaidi wa kiuchumi dhidi ya taifa la Iran kwa kuzidisha vikwazo vya kimataifa na kuzichochea nchi nyingine zitekeleze vikwazo hivyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata hivyo, vikwazo vya Washington dhidi ya Iran si tu kwamba havijapata matokeo yaliyotarajiwa na Marekani, bali vimethibitishwa kutokuwa na makali wala taathira yoyote ya maana dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran. Nchi ambazo kwa kawaida huwekewa vikwazo na nchi za Magharibi, na hasa Marekani, ni zile zinazofuata siasa uhuru katika ngazi za kimataifa, jambo ambalo huikera sana nch hiyo ya kibeberu. Hii ndio maana Washington inatekeleza siasa kandamizi na za uburuzaji kupitia vikwazo dhidi ya mataifa yenye siasa huru duniani na hasa Iran, kwa ajili ya kulinda maslahi yake haramu katika ngazi za kimataifa. Kuendelea mwenendo huo kunaonyesha kuwa Marekani haijaweza kufikia malengo yake kupitia vikwazo na ndio maana inavizidisha kama ishara ya kudhihirisha hasira na wakati huo huo kuonyesha kukata tamaa. Hasa ikitiliwa maanani kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyo huru inazidi kusonga mbele na kupata mafanikio makubwa katika njia hiyo, jambo ambalo limezifanya nchi nyingine duniani pia kushawishika kufuata njia hiyo hiyo na hivyo kujiondoa kwenye minyororo ya ubeberu wa Marekani.

342/