Main Title

source : Parstoday
Jumanne

19 Machi 2024

14:35:53
1445554

Abdollahian: Iran ina azma ya kuimarisha uhusiano na Niger

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa serikali ya Rais Ebrahim Raisi ina hamu ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na nchi za Afrika ikiwemo Niger.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema hayo katika mazungumzo yake na balozi mpya wa Iran nchini Niger, Ali Tiztak kabla ya mwakilishi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu kuondoka nchini kwenda katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Abdollahian amebainisha kuwa, kuna haja ya kufuatiliwa makubaliano yaliyosainiwa baina ya Iran na Niger kwa ajili ya kuharakisha mchakato wa utekelezaji wake, hasa kupitia kamisheni za pamoja za uchumi za nchi mbili hizi.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ametilia mkazo suala la kuimarishwa zaidi uhusiano wa kiuchumi na kisiasa baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Niger, pamoja na nchi nyingine za Afrika.

Amesema serikali ya 13 Jamhuri ya Kiislamu chini ya urais wa Rais Ebrahim Raisi inalipa kipaumbele kikubwa suala la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi za Afrika na kusisitiza kuwa, ni jukumu la wawakilishi wa Iran nje ya nchi kutumia hadhi zao za kidiplomasia kusaidia kuimarisha mahusiano ya kibiashara baina ya Iran na bara hilo.

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria ulazima wa kubadilishwa mitazamo kuhusu bara la Afrika na kuzingatia fursa nyingi na tofauti zinazopatikana katika bara hilo.

Kabla ya kuteuliwa kuwa balozi wa Iran nchini Niger, Ali Tiztak amewahi kuhudumu katika nyadhifa tofauti huko nyuma. Amewahi kuwa Mkuu wa Sekritarieti ya Bahari ya Caspian, naibu balozi wa Iran nchini  Turkmenistan, mbali na kuhudumu katika balozi za Iran huko Moscow na Kiev.

342/